Wamuomba Rais Samia kuingilia kati sakata la Bonde la Msimbazi

Muktasari:
- Wananchi wa Magomeni Suna watakaoathiriwa na mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi wamtaka Rais Samia kuingilia kati madai malipo ya fidia.
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya waathirika wa mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi, wakilalamika kutofanyiwa tathimini wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili waweze kupata haki yao.
Kilio cha wakazi hao kinakuja ikiwa ni siku chache tangu Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamisemi) kutangaza kuanza kusainisha mikataba ya malipo ya fidia pamoja na kuhakikiwa taarifa za benki kabla ya kufanyiwa malipo.
Kwa nijibu wa tangazo hilo shughuli hiyo itaenda sambamba na wale ambao hawakuridhika na uthamini kuthaminiwa upya kwa kuzingatia aina ya malalamiko yao.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 wanakazi hao wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili waweze kulipwa fidia zao kulingana na tathimini.
"Katika malipo ya fidia kumetokea utata, tumevunjiwa nyumba tangu 2016 Kwa kuwa sina sehemu ya kulala hatujui tuende wapi tumeathirika kisaikolojia," amesema Desideri Silayo.
Alisema maeneo hayo walifanyiwa tathimini lakini hawana uhakika wankulipwa baada ya kutokuona majina yao na kumuomba Rais Samia kuingilia kati.
"Rais atuangalie kwa jicho la huruma wapo watu ambao majengo yao hayajaonekana, zaidi ya watu 400 tulivunjiwa katika uthamini ni baadhi tu ya nyumba zimeonekana," amesema Silayo.
Mkazi mwingine Anitha Makanza alisemakwenye tathimini nyumba yake imerukwa na katika watu wanaotakiwa kulipwa fidia haoneekani.
Alisema amekuwa akiishi katika eneo hilo tangu mwaka 1980 na wamekuwa wakilipa kodi zote za Serikali.
"Tunasikia wanataka kurudia kufanya tathimini tunawangija waje ingawa hatujapewanmuda wa kuondoka,"amesema Makunza.
Kwa upande wake mkazi mwingine Abdalah Said alisema walivunjiwa nyumba zao lakini wanashangaa kwanini hawalipwi.
Alisema wanamtaka Rais Samia kuwasikiliza maoni yao Kwa kuwa wamekuwa wakuteseka na kunyanyasika.
"Rais anapaswa kukutana na sisi na kutusikiliza, viongozi waliopo sijui ni kwa maslahi gani tunaomba msaada wake,” amesema.
"Kwa tathimini iliyofanyika hawataki kutulipa wanataka kulipa nyumba walizozikuta na wakati kuna kipindi walituvunjia," amesema Said.
Alibainisha kuwa wamekuwa wakilipa kodi mbalimbali ikiwemo Kodi za majengo, pamoja na huduma zote muhimu.
"Uthamini uanze upya haya ni matatizo wakati mwingine hatuelewani wenyewe Kwa wenyewe tunaomba serikaali itusimamie tupate haki yetu," amesema.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Serikaali ya Mtaa wa Suna, Salum Hamis alikiri kuwepo malalamiko hayo akidai yeye siyo msemaji.
Amesema malalamiko hayo hayajaanza leo kwani iko kamati inayoshughikia suala hilo na yeye ni mjumbe.
"Malalamiko haya ni kweli yapao mimi sina ufafanuzi iponkamati iliyoundwa nadhani wako Kwa mkuu wa Wilaya hao ndio wenye ufafanuzi," amesema Hamis.
Kutekelezwa Kwa mradi huo wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi, utazuia mafuriko na kuhusisha ujenzi wa daraja la juu katika Barabara ya Morogoro pamoja na ujenzi wa kingo katika bonde la mto huo utakaogharimu zaidi ya Sh598 milioni.
Taarifa ya usainishwaji wa mikataba hiyo ilitolewa Jumamosi Oktoba 14,2023 kwenye tangazo la Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-Tamisemi).
Tamisemi inatekeleza mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kwa lengo la kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde, kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha serikali kuingiza zaidi ya Sh2 trilioni.
Hata hivyo, ili kufanikisha utekelezaji wa mradi serikali inatarajia kuwahamisha watu wote wanaoathirika na mradi kwa kuwalipa fidia za mali zao zinazoathirika.
Katika tangazo hilo, Katibu Mkuu alisema shughuli ya ulipaji fidia inatarajiwa kuanza Oktoba 20 na itafanywa na Kampuni ya Property Matrix Limited kwa niaba ya Tamisemi.
Taarifa hiyo iliorodhosha ratiba kuwa Oktoba 18 hadi Oktoba 20 watasainishwa watu wa Kata ya Mchikichini katika ukumbi wa DRIMP-Ilala Kota, ikihusisha Mtaa wa Msimbazi Bondeni.
Oktoba 21 hadi Oktoba 22, watakaosainishwa ni wakazi wa Kata ya Mchikichini mtaa wa Misheni Kota na Ilala Kota.Wengine wataosanishwa tarehe hizo ni Kata ya Kariakoo, Mtaa wa Kariakoo Kaskazini.
Oktoba 23 hadi Oktoba 25, watasainishwa ni Kata ya Magomeni mtaa wa Suna shughuli itakayofanyika ofisi ya Kata Magomeni, ikifuatiwa na Kata ya Mzimuni Oktoba 26 ambapo watasainishwa pia Mtaa wa Idrisa, Mtambani na Mwinyi Mkuu katika ofisi ya Kata Mzimuni.
Ratiba nyingine ni Oktoba 27 hadi Oktoba 28, watakaosainishwa ni Kata ya Kigogo ikihusisha mtaa wa Kigogo Mbuyuni na Oktoba 29 hadi Oktoba 30 watasainishwa Kata ya Hananasif ikihusisha mitaa ya Mkunguni A, Mkunguni B na Hananasif, shughuli itakayofanyika Shule ya Msingi Mapinduzi-Kigogo.
Oktoba 31 hadi Novemba 2, watasainishwa Kata ya Upanga Magharibi, Mtaa wa Charambe, Kata ya Jangwani mitaa ya Mtambani A, Mtambani B na Jangwani..Mtaa wa Kawawa watasainishwa kuanzia Novemba 3 hadi Novemba katika Ukumbi wa DRIMP Ilala Kota.