Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitendawili malipo kwa wakazi wa Bonde la Msimbazi

Muktasari:

  • Zoezi la kuwasainisha mikataba ya malipo ya fidia pamoja na kuhakiki taarifa kwa waathirika wa mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi wamegawanyika makundi mawili wapo wanaokubali na wapo wanapinga fidia hiyo.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikianza kuwasainisha mikataba ya malipo ya fidia pamoja na kuhakiki taarifa za kibenki kwa waathirika wa mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi, baadhi yao wameamua kusaini huku wengine wakigoma kwa madai ya kutokubaliani na viwango vya fidia.

Shughuli ya kuwasainisha mikataba pamoja na uhakiki wa mali zilizoathirika na mradi huo, ilianza jana kufuatia tangazo la Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) akiwataka wahusika kufika kwenye maeneo yaliyoainishwa.

Makundi yanayohusika kwenye shughuli hiyo ni wale waliotia saini uthaminishaji uliofanyika Machi, mwaka huu na wale ambao walikataa kutia saini uthaminishaji huo kwa madai kwamba walichothaminiwa hakilingani na thamani ya mali zao.

Leo, mamia ya wananchi walijitokeza kwenye utiaji saini wa mikataba ya malipo katika wilaya ya Ilala ambapo baadhi yao wakilalamikia kutolipwa fidia wanayostahili na pia ardhi kutojumuishwa kwenye fidia watakayolipwa.

Mkazi wa Msimbazi Bondeni, Amina Shelufumo alisema wakati wa uthaminishaji alitia saini lakini akaambatanisha na malalamiko yake ya kutoridhishwa na kiasi alichothaminiwa, hata hivyo alipokwenda leo alikuta kimeongezeka lakini kidogo.

“Mimi nimekataa kusaini kwa sababu nitalipwa kiasi kidogo ambacho hakiendani na mali zangu. Nilithamniwa kulipwa Sh11 milioni lakini leo nimekuta ni Sh15 milioni, nimekataa kusaini, bado ni kiasi kidogo,” alisema mwanamke huyo.

Kwa upande wake, Mariam Sozigwa alisema ameishi Jangwani kwa miaka 16, sasa anaambiwa ahame kwa kulipwa Sh5 milioni, kiasi ambacho alisema hawezi kufanya jambo lolote hasa katika umri wake wa uzee.

“Sh5 milioni nitafanyia nini, inatosha kujenga nyumba nyingine? wanataka niende nikapange katika umri huu? Hii siyo haki kabisa, tunataka watulipe kiasi ambacho tunaweza kujenga nyumba nyingine kwa sababu tumepoteza nyumba zetu,” alisema Sozigwa.

Hata hivyo, mkazi wa Msimbazi Bondeni, Mukhtar Bilaly alisema licha ya kwamba kiasi wanacholipwa hakitoshi, ameamua kusaini ili amalize jambo hilo na kutafuta uelekeo mwingine wa maisha.

“Serikali ikiamua jambo huwezi kupingana nalo, mimi nilijifunza walichofanyiwa watu wa Mbezi kipindi kile, walivunjiwa nyumba zao bila fidia. Kwa hiyo nimeona nisaini hiki kidogo nilichopewa,” alisema Bilaly.

Bilaly aliongeza kwamba katika fomu ya mkataba aliyosaini, ameelekezwa kwamba ndani ya wiki sita baada ya kulipwa stahiki zake, atatakiwa kuhama katika eneo lake kupisha mradi huo katika Bonde la Msimbazi.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi hao, ofisa mmoja wa Tamisemi ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alibainisha kwamba watakaoathirika na mradi huo ni watu 2,592, kati ya hao, 167 walikataa kujaza fomu za uthamini na wengine 211 hawakupatikana wakati wa uthamini.

Alisema baada ya kufanyika kwa uthaminishaji, orodha ilipelekwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali ambaye naye alituma timu yake kwenda kujiridhisha na baadaye kupitisha uthamini uliokuwa umefanyika.

“Hawa tunaowasainisha leo, taarifa zao za uhakiki zilishathibitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali, kwa hiyo kama hawajakubaliana na uthamini, basi watakata rufaa kwa Mthamini Mkuu,” alisema ofisa huyo.

Aliongeza kwamba wale ambao waligoma kusaini kwa sababu hawakuafiki viwango vya fidia walivyokadiriwa, watafanyiwa tathmini upya kwenye maeneo yao ili kujiridhisha na kupata thamani halisi ya kile wanachostahili kulipwa.

Kuhusu ardhi kutolipwa fidia, ofisa huyo alibainisha kwamba eneo la Jangwani halijapimwa na halina GN, hivyo hawastahili kulipwa chochote kwa mujibu wa sheria, lakini kwa huruma ya Serikali, wote watalipwa kiasi fulani kinachofanana.

“Kulikuwa na uchaguzi wa kulipwa fidia, asilimia 98 walisema wanataka fedha, lakini wengine (asilimia 2) walisema wanataka wafidiwe viwanja na wengine wakataka wapewe sehemu za kuishi baada ya mradi kukamilika,” alisema ofisa huyo.