Yanga, Azam kisasi VPL

New Content Item (1)
Yanga, Azam kisasi VPL

Muktasari:

Timu ya Azam FC na Yanga SC zinakutana leo katika mechi ya kisasi na kulinda heshima ambayo kila upande utataka kuweka rekodi na kumshusha mpinzani wake katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Dar es Salaam. Timu ya Azam FC na Yanga SC zinakutana leo katika mechi ya kisasi na kulinda heshima ambayo kila upande utataka kuweka rekodi na kumshusha mpinzani wake katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo kati ya timu hizo utafanyika katika Uwanja wa Azam Complex - Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka nchini kutokana na rekodi za timu hizo baina yao, inazikutanisha kila moja ikiwa na pointi 25 kwenye msimamo, lakini Azam iko kileleni kutokana na kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa hivyo yoyote itakayoshinda itaongoza ligi.

Sare ya bao 1-1 iliyopata Yanga Jumapili dhidi ya Namungo imeongeza mvuto wa mechi ya leo kwani Azam nayo iliangukia pua Jumamosi kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KMC, hivyo kila timu haitakubali rahisi kupoteza mchezo leo.

Timu hizo zinakutana zikiwa na presha ya kupata ushindi kwani mpinzani wao mkubwa Simba yenye pointi 23 inawafuatia kwa kasi, licha ya kwamba wiki hii haitacheza mchezo wa ligi kutokana na kukabiliwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Plateau ya Nigeria.

Rekodi Azam, Yanga balaa

Tangu Azam ipande Ligi Kuu msimu wa 2008/2009 imekutana na Yanga mara 24 kwenye ligi, ikishinda mara nane sawa na wapinzani wao huku zikitoka sare mara nane.

Azam imeonekana kuwa vizuri kwenye ufungaji ikiwa na mabao 29 wakati Yanga ikifunga 28, huku mshambuliaji John Bocco anayeichezea Simba kwa sasa ndiye aliyezitikisa nyavu za Yanga mara nyingi - akifunga mabao 10 wakati akiichezea Azam.

Pia, Azam imepata ushindi dhidi ya Yanga wa mabao zaidi ya mawili mara nyingi kuliko wapinzani wao ikifanya hivyo mara tatu wakati Yanga ikishinda mabao matatu dhidi ya Azam mara moja.

Yanga iliwahi kuifunga Azam 3-1 katika mchezo uliofanyika Oktoba 15, 2008 na tangu hapo haijashinda tena kwa idadi kubwa ya mabao dhidi yao.

Hata hivyo, Yanga imewahi kuifunga Azam kwa mabao mengi katika mchezo wa Ngao ya Hisani uliofanyika Septemba 16, 2014 iliposhinda mabao 3-0 na pia Mei 25, 2016 ilipoifunga 3-1 katika Kombe la Shirikisho (FA).

Azam imekuwa ikiipa kipigo cha mabao mengi Yanga katika mashindano tofauti, kwani tangu 2010 katika Ligi Kuu imeichapa kuanzia mabao matatu katika mechi tatu. Iliifunga mabao 3-1 Machi 10, 2012, kisha ikaichapa mabao 3-2 Septemba 22, 2013 na iliifunga mabao 3-1 Mei 28, 2015.

Pia, imewahi kuifunga Yanga mabao 4-0 katika Kombe la Mapinduzi Januari 7, 2017 na vilevile mabao 3-0 katika mchezo wa mashindano hayo uliofanyika Januari 5, mwaka jana.

Wasikie makocha

Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze alisema jana kuwa yupo tayari kuikabili Azam huku akidai itakuwa mechi kali na ngumu.

“Tuko tayari kwa Azam, itakuwa mechi kali sana lakini nina uhakika matokeo yatakuwa mazuri kwetu,” alisema Kaze.

Naye kocha msaidizi wa Azam, Vivier Bahati alisema sare ya Yanga dhidi ya Namungo imewapa ahueni ingawa mchezo utakuwa mgumu.

“Muhimu ni kusahihisha makosa ya mchezo uliopita na kuhakikisha wa leo tunafanya vizuri na kuibuka na ushindi ili tuendelee kubaki kileleni,” alisema Bahati.