Zaidi ya kaya 40 zazingirwa na maji Siha

Baadhi ya nyumba zilizozingirwa na maji katika Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Muktasari:

 Serikali ya Wilaya ya Siha imesema kwa sasa wanaendelea kuangalia maeneo mbalimbali kuona kama kuna madhara mengine

Siha. Kaya 40 zimezingira na maji katika Kijiji cha Wiri kilichopo Kata ya Gararagua, wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro baada ya mvua kubwa kunyesha jana na kusababisha mafuriko.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo, Aprili 14, 2024, Mkuu wa Wilaya Siha, Dk Christopher Timbuka amethibitisha kutokea kwa maafa hayo na kuwataka wananchi waliopo maeneo hayo kuondoka na kutafuta sehemu salama za hifadhi.

Amesema pamoja na wananchi kuzingirwa na maji, pia miundombinu ya barabara imeharibiwa na mvua hizo yakiwamo madaraja.

“Ni kweli kuna maeneo nyumba zimezingirwa na maji kikiwamo Kijijii cha Wiri, tumewashauri wananchi watafute sehemu salama za kwenda kwa sababu hatuwezi kujua mvua zitanyesha hadi lini, mvua zikiendelea kunyesha, hali itakuwa ngumu zaidi kuondoka,” amesema Dk Timbuka.

Amesema kwa sasa wanaendelea kuangalia maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kuona kama kuna madhara mengine yamejitokeza.

“Kwa sasa nipo Kijiji cha Embukoi, naendelea na ziara kuangalia athari za mvua hizi ambazo zimenyesha maeneo mbalimbali ya wilaya yetu,” amesema Dk Timbuka.

Akizungumzia athari za mvua hizo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wiri, Hamza Munisi amesema kaya 40 zimezingirwa na maji kijijini hapo na wanafanya jitihada za kuwatafutia maeneo mengine yalioathirika na mafuriko hayo wakati wakisubiri utaratibu mwingine wa Serikali.

“Kuna kaya 40 hapa kijijini kwangu zimezingirwa na maji, jana mvua kubwa imenyesha na kutuletea maafa ila tunafanya jitihada za kuwahamasisha wananchi waondoke katika maeneo haya wakati tukisubiri utaratibu wa Serikali,” amesema mwenyekiti huyo.

Katika tukio jingine, mvua zinazoendelea kunyesha katika Kijiji cha Embukoi, zimesababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya kijiji hicho na kijiji cha jirani kutokana na daraja linalounganisha vijiji hivyo kuathiriwa na maji ya mafuriko.

Akizungumzia athari za mvua, mwenyekiti wa Kijiji cha Embukoi, Mathayo Lengere amesema daraja linalounganisha kijiji hicho na kijiji cha Mungushi wilayani Hai, limeharibiwa vibaya kingo zake na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara.

“Hili daraja ni muhimu kwetu, mbali na watu kulitumia kwenda Bomang'ombe wilayani Hai kwa shughuli mbalimbali, pia kuna wanafunzi wanatoka Kijijii cha Mungushi wilayani Hai kwenda Shule ya Sekondari Sekirari iliyopo Kijiji cha Embukoi ambapo kwa sasa hawawezi kupita,” amesema Mathayo.

Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa taarifa zaidi.