Mafuriko yasimamisha shughuli za uzalishaji mali Ulanga, Tazara ikipambana kurejesha safari za Dar- Mbeya
Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu (mwenye fulana ya mistari) akizungumza na wakulima na wavuvi wa kitongoji cha Itoo na Mkwajuni kata ya Minepa wilayani humo ambao nyumba zao zimezingirwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha . Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu amefunga Shule ya Msingi Kivukoni A na kuwataka wavuvi kuondoka kwenye kambi zao hadi maji yatakapopungua.
Ulanga. Ulanga. Serikali imelazimika kuifunga Shule ya Msingi Kivukoni A iliyopo Kata ya Minepa Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, baada ya kuzingirwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo na kusababisha mafuriko. Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 9,2024 Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu amesema wameifunga shule hiyo kwa siku 15 kwa usalama wa wanafunzi.
"Tumeifunga jana baada ya kuona hali sio nzuri, pamoja na kwamba tumeweka siku 15, hata hivyo tutaangalia hali ya hewa kama mvua zitaendelea basi itabidi tuwahamishie wanafunzi kwenye shule ya msingi Kivukoni B na tutaanza kuwahamisha wanafunzi wa darasa la nne na la saba ambao wanategemea kufanya mtihani mwaka huu," amesema Dk Ningu.
Kuhusu miundombinu, amesema bado usafiri wa barabara ni changamoto baada ya barabara kuu ya kutoka Ifakara kwenda Ulanga na zile za ndani kuharibika na nyingine kushindwa kupitika kwa usafiri wa magari madogo.
Hata hivyo, amesema tayari wataalamu kutoka Wakala wa Barabara (Tanroad) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wameshafika kurekebisha maeneo yaliyoathiriwa.
"Hali ya barabara zetu sio nzuri, lakini tunashukuru wenzetu wa Tanroad na Tarura wamekuja na mitambo na magari makubwa yanayofanyakazi ya kuvuta magari yanayokwama yakiwamo mabasi,” amesema.
Mkuu huyo wa wilaya ametaja shughuli zilizoathiriwa na mafuriko hayo ni pamoja na za kilimo, baada ya mashamba kujaa maji, huku shughuli za uvuvi zikisimama kutokana na mito kujaa maji pia.
"Kambi mbili za wavuvi na wakulima wa mpunga za Itoo na Mkwajuni ziko kwenye maji na nimeagiza waondoke haraka, nashukuru taarifa nilizopewa ni kuwa wameshaanza kuondoka,” amesema Dk Ningu.
Amesema baadhi ya majengo ya Serikali zikiwamo ofisi za vijiji, kata nazo zilizingirwa na maji, lakini kwa sasa maeneo hayo yameamza kupungua na baadhi shughuli za kuwahudumia wananchi zinaendelea kama kawaida.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa maeneo ya Ifakara na Mlimba wilayani Kilombero nako hali imeanza kurejea kama ilivyokuwa awali baada ya maji kuanza kupungua.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema wataalamu wa Tanroad na Tarura bado wanaendelea na kazi ya kurekebisha madaraja na miundombinu ya barabara ya kutoka Ifakara -Mngeta hadi Mlimba.
Amesema Serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kupeleka misaada ya ikiwamo ya vyakula ili kuwanusu na njaa wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo.
Naye Mkuu wa Stesheni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) Mlimba, Alex Mhiri amesema usafiri wa treni wa Mbeya - Dar es Salaam bado haujaanza kwa kuwa njia haijafunguliwa kutokana na matengenezo ya reli yanayoendelea, baada ya kifusi kuporomoka na kuziba njia wiki moja iliyopita.
Mhiri amesema safari zilizoanza ni zile za kutoka Mlimba - Dar es Salaam na treni imekuwa ikifanya safari siku za Jumanne na Alhamisi.
"Leo ni siku ya tatu mvua haijanyesha huku Mlimba na tunaamini kama hali itakuwa hivi kwa muda wa wiki moja, kazi ya kufungua njia itakuwa imemalizika," amesema Mhiri.