Zaidi ya tani 200,000 za korosho zasafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara

Baadhi ya wadau wakiwa kwenye mkutano wa ushoroba wa maendeleo ya Mtwara ulioandaliwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara amesema usafirishaji wa korosho kupitia Bandari ya Mtwara umefanyika kwa mafanikio makubwa

Mtwara. Tani 244,680 za korosho ghafi zenye thamani ya Sh454 bilioni zimezalishwa nchini huku tani 229,544 zikisafirishwa nje ya nchi kwa kutumia Bandari ya Mtwara katika msimu wa mwaka 2023/24 huku minada 55 ikifanyika nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo wa ushoroba wa Mtwara leo Aprili 18 2024, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara amesema usafirishaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa.

Amesema TPA imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Septemba 2023 la kusafirisha korosho za mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Bandari ya Mtwara.

“Bandari yetu imefanyiwa maboresho makubwa sambamba na kuongeza vifaa vyenye nguvu ili kufanya kazi kwa ufanisi na tumeleta mashine za kupakia na kupakua mizigo na kuongeza idadi ya wafanyakazi katika bandari hiyo,” amesema Kijavala.

Akiwasilisha taarifa ya msimu wa korosho, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Masoko na Udhibiti wa Ubora wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Revelian Ngaiza amesema zaidi ya tani 244,680 zimezalishwa nchini na tani 144,018 zimekusanywa ndani ya Mtwara.

“Tulifanya zaidi ya minada 55 ya korosho ghafi nchi nzima kupitia vyama vya ushirika, zaidi ya tani 244,680 za korosho ghafi zilikusanywa na kuuzwa huku tani 229,000 zikisafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara ambazo zilitoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma,” amesema Ngaiza.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Viwanda na Wakulima, Kizito Galinoma amesema mbali na maboresho yaliyofanikisha korosho kupita Bandari ya Mtwara kupitia ushoroba, wanaomba ujenzi wa reli uzingatiwe na bandari iboreshwe zaidi.

 “Unajua bandari haikupitisha korosho kwa zaidi ya miaka mitano, kitendo cha kupitishia hapa kwetu ni faraja, pamoja na changamoto mbalimbali hasa vifaa lakini tuliweza kufanikisha jambo hilo,” amesema Galinoma.