Bodi ya Korosho yawaonya wafanyabiashara wanaozitorosha nje ya nchi

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred amesema wapo wanunuzi wanaonunua korosho baada ya msimu kufungwa na kutaka kuzisafirisha kwenda nje ya nchi kinyume cha utaratibu.

Mtwara. Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imewaonya baadhi ya wanunuzi wa zao hilo  wanaonunua baada ya msimu kufungwa na kutaka kuzitorosha nchini kinyume cha sheria.

Amesema hadi sasa  kampuni mbili zimechukuliwa hatua na kutozwa faini ya zaidi ya Sh45 milioni. 

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya uzalishaji wa korosho msimu wa mwaka 2023/2024, kilichofanyika leo Aprili 7, 2024, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred amesema wapo wanunuzi wanaonunua korosho baada ya msimu kufungwa na kutaka kuzisafirisha kwenda nje ya nchi kinyume cha utaratibu.

Amesema korosho zinazoruhusiwa kwenda nje ni zile zilizonunuliwa wakati wa minada, zilizonunuliwa baada ya minada kufungwa ni kwa ajili ya viwanda vya ndani ya nchi pekee.

Hata hivyo, Alfred amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna kibali chochote kitakachotolewa kwa ajili ya kusafirisha korosho kwenda nje ya nchi. 

“Hatutoi vibali kwa mtu yeyote wala viwanda, korosho zilizobaki zitabanguliwa hapahapa nchini, nawatahadharisha wote wanaonunua kinyume cha utaratibu, tutawachukulia hatua, hata juzi tumekamata gari moja likiwa na tani 38, wamenunua kinyume cha utaratibu na hawakuwa na vibali. “Tumewatoza faini zaidi ya Sh25 milioni, pia, kuna kampuni moja ilitaka kutorosha korosho kwenda Dar es Salaam zikiwa hazina vibali, nao tuliwatoza faini Sh20 milioni,” amesema Alfred.

Amesisitiza kwamba: “Nataka niwatahadhalishe wote wanaojaribu kuchukua korosho kinyume cha utaratibu wataingia hasara. Endapo kuna mtu ama kampuni inataka kununua korosho sasa hivi lazima uzibangue hapahapa nchini.”

Alfred amesema walianzisha soko la awali ili kuongeza ubanguaji ndani ya nchi ambapo nchi nyingi zinazolima korosho huwa zinaruhusu wabanguaji wa ndani kununua zao hilo kupitia kwa wakulima, ambapo usimamizi wake upo kwenye Bodi ya Korosho, halmashauri na vyama vya ushirika katika ngazi za Amcos.

“Katika mfumo huu, naona changamoto kubwa ni wadau wanaohusika kwenye ule mwongozo kutotekeleza wajibu wao ipasavyo, tumekubaliana kuwa tunaenda kuboresha baadhi ya vipengele ili kuziba mianya ya watu wanaoitumia vibaya soko la awali,” amesisitiza Alfred.

Kwa upande wake, meneja ubanguaji wa CBT, Mangire Maregesi amesema wakati msimu unaanza yapo yaliwekwa ambayo ni kuzalisha tani 400,000 na kubangua tani 42,000 ambapo hadi sasa zaidi ya tani 20 zimeshabanguliwa nchini.

“Hadi kufikia Agosti ndiyo tutaangalia tumefikia wapi, kwa sasa tunaendelea kukusanya takwimu kwa kuwa bado kuna korosho nyingi kwenye majumba ya watu, tunahitaji kukusanya hizo takwimu ili kuhakikisha kuwa tumepata takwimu halisi za uzalishaji na ubanguaji ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya tani 100,000 bado zipo nchini,” amesema Maregesi.

Mwakilishi wa Taasisi ya Wabanguaji Wakubwa wa Korosho (TACP), Jamal Kamtwanje amesema soko la awali limeongeza fursa nyingi ikiwemo kumuwezesha mlaji kufahamu korosho anazokula zimetokea nchini gani, na wawekezaji wapya kuja na kuongeza ajira nchini.

“Soko hili linamwezesha mlaji kujua korosho zilipotoka, ni mfumo wenye manufaa ingawa kuna changamoto kwenye kufahamika kwa mfumo huu na wengi hawafahamu namna ulivyo. Ni vema watendaji wakafuatilia miongozo inayotolewa na CBT kwa kila msimu ili kujua unataka nini na kufuata utaratibu,” amesema Kamtwange.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kiwanda cha kubangua korosho cha Amamas Farmer, Ammar Jiwaji amesema soko la awali limeongeza ajira kwa viwanda viwili vya Tandahimba na Mkuranga ambapo wameajiri zaidi ya watu 1,200 na kuongeza goli la ubanguaji na kwa mwaka huu wanatarajia kubangua tani 7,000 ambazo zinasafirishwa kwenda nchi mbalimbali duniani.

“Soko la awali linasaidia kulinda ajira za Watanzania na kupunguza mzunguko wa korosho kusafirishwa umbali mrefu, kwa msimu ujao tunatarajia kubangua zaidi ya tani 7,000 ambapo zaidi ya watu 1,200 wameajiriwa katika viwanda vyetu,” amesema Jiwaji.