Wakulima wa korosho walilia ubanguaji kuongeza tija

Muktasari:
- Bei ndogo ya korosho kwenye minada ya mwaka huu imewalazimu wakulima wa korosho nchini kutaka kuongeza ubanguaji ili kupunguza usafirishaji wa korosho ghafi, suala litakalowaongezea kipato hata ajira kwa vijana nchini.
Bei ndogo ya korosho kwenye minada ya mwaka huu imewalazimu wakulima wa korosho nchini kutaka kuongeza ubanguaji ili kupunguza usafirishaji wa korosho ghafi, suala litakalowaongezea kipato hata ajira kwa vijana nchini.
Katika kufanikisha hilo, wameiomba Serikali kuvifufua viwanda 12 vilivyobinafsishwa awali pamoja na kujenga vipya sambamba na kuingiza vifungashio bora vitakavyokubalika katika soko la ndani hata kimataifa.
Said Issa, mkulima wa korosho wa Nanganga wilayani Masasi anasema litakuwa jambo la busara iwapo Serikali itavifufua viwanda vilivyobinafsishwa miaka ya nyuma.
“Kubangua korosho kulikuwepo tangu zamani lakini tukashangaa vinafungwa. Siku zote tunalilia korosho zibanguliwe hapahapa nchini. Vilipokuwepo viwanda maslahi ya korosho yalionekana sana.” Mkulima mwingine, Sofia Abdallah wa Nanganga anasema wapo tayari kubangua korosho iwe kwa mashine za nyumbani au kuzipeleka kiwandani iwapo vitafufuliwa au kujengwa vipya, kwani ndio namna pekee wanayoamini itawaongezea kipato.
“Changamoto iliyopo ni kwamba hatuna viwanda na hatuwezi kukaa na korosho ndani kwa muda mrefu, matokeo yake tunauza ikiwa ghafi hata kwa bei ya hasara,” anasema Sofia.
Hamu ya kuwa na viwanda vitakavyobangua korosho inayolimwa nchini haipo kwa mkulima mmojammoja tu, bali jamii hasa za mikoa ya kusini inayoongoza kwa kilimo hicho kwa sasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Amani wilayani Masasi, Abdillah Said anasema wanaomba viwanda vipatikane vijijini ambako baadhi ya watu wanabangua kwa njia za asili ili waachane na utaratibu wa kupeleka maghalani korosho ghafi.
“Serikali iweke msimamo kwenye suala la viwanda ili watu wabangue, bei tunayoipata kwa kuuza korosho ghafi ni ndogo sana,” anasema Said.
Hata Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi, Mtwara na Nanyumbu (Mamcu), Bihadia Matipa anasema kuvifufua viwanda vilivyobinafsishwa ni wazo zuri na hicho kilikuwa kilio chao cha siku nyingi.
“Serikali inalifanyia kazi hilo na wametuahidi viwanda vitafufuliwa ili korosho yetu yote ibanguliwe nchini. Hii likifanyika, kipato cha mkulima kitaimarika. Kati ya viwanda vitakavyofufuliwa, viwili ni vya Mamcu vilivyopo Masasi na Mtwara,” anasema Bihadia.
Mipango ya Serikali
Kilio cha wakulima hawa kimekuja siku chache baada ya kushuhudia minada ya kwanza ya msimu huu wa mavuno ikiwa na bei ndogo iliyowalazimu kugoma kuuza mavuno yao.
Akizungumza na wananchi wakati Rais Samia Suluhu Hassan anawasalimia wakazi wa Mtwara mjini akitokea Lindi kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) inatarajia kutangaza zabuni ya kununua mashine ndogo za ubanguaji zitakazosambazwa bure kwa wakulima.
Kwa kutumia mashine hizo ndogondogo, Bashe alisema wakulima wataweza kubangua korosho katika makazi yao, huku mzigo mkubwa zaidi ukichakatwa viwandani kwani Serikali imeanza kujenga kiwanda cha kwanza wilayani Newala na inaongea na wawekezaji ili kuvifufua viwanda 12 vilivyobinafsishwa na kufa ili vianze ubanguaji.
“Changamoto iliyokuwapo ilikuwa kutokuwa na uhakika wa soko, lakini tayari tumeshapata ithibati ya kimataifa ya kubangua, kufungasha (packaging) na kuuza korosho nje, hivyo kilichobaki ni utekelezaji tu,” alisema Bashe.
Bashe alitoa ufafanuzi huu baada ya Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota kuiomba Serikali kufufua viwanda vya kubangua korosho ili viwe mwarobaini wa bei ndogo wanayolipwa wakulima.
“Uchumi wa Mtwara unategemea korosho, lakini kuporomoka kwa bei kwenye minada imekuwa changamoto ya kila siku kwa wakulima wa zao hili,” alisema Chikota.
Katika ufafanuzi wake, Waziri Bashe alisema bei ya korosho imeshuka duniani kote na akatolea mfano nchini Msumbiji kwamba kilo moja ya korosho ghafi inauzwa kati ya Sh1,000 hadi Sh1,200 hata Gambia, Ghana na Ivory Coast ni chini ya dola moja ya Marekani (Sh2,300) kwa kilo.
“Kwa hiyo njia pekee ni sisi kuanza ubanguaji. Kuanzia mwakani tutagawa vifaa vya kubangulia kwa wakulima sambamba na kuvifufua viwanda hivi ili tuuze korosho iliyobanguliwa,” alisema Bashe.
Mafanikio ya mpango huo alisema yameanza kuonekana, kwani kwa mara ya kwanza mwaka huu, tani saba za korosho zilizobanguliwa kutoka wilayani Tandahimba zimesafirishwa kwenda nchini Marekani.
Ili kuongeza zaidi uwazi, alisema kuanzia mwakani minada itakuwa inafanyika kwenye maeneo ya wazi waliko wakulima.
Serikali imeeleza hatua hizo kipindi ambacho Tanzania inatarajia kuanza kuvuna kiasi kikubwa cha korosho baada ya kilimo chake kuenezwa katika mikoa mingine mipya 17 ambako mazingira yameonyesha yanakubali kilimo hicho.
Kutokana na wastani wa tani 300,000 ambazo imekuwa ikivuna kila mwaka, Tanzania inatarajia kuanza kupata zaidi ya tani milioni moja kuanzia msimu wa mwaka 2025, huku kiasi kikubwa kikibanguliwa nchini tofauti na hali iliyopo ambapo zaidi ya asilimia 80 huuzwa ghafi kwenda nchi za nje.
Viwanda vilivyopo kwa sasa vina uwezo wa kubangua takriban tani 100,000, lakini huwa vinapata wastani wa tani 30,000 kutokana na ushindani uliopo kwenye minada inayofanyika kwa kuzihusisha kampuni za kimataifa zenye mtaji mkubwa.
“Ni suala linalohitaji utashi na utayari wa kisiasa tu. Kwanza viwanda vilivyopo viwekewe mazingira ya kupata malighafi za kutosha mwaka mzima wakati vipya vikiendelea kufufuliwa au kujengwa. Korosho ndilo zao linaloipa Serikali fedha nyingi za kigeni, linahitaji mkakati mahsusi,” amesema Yohana Charles, mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi.
Uchumi mbadala
Licha ya kuongeza thamani ya korosho nchini, Waziri Bashe ameahidi kuongeza vyanzo vya mapato kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwa kuwatanulia fursa kwenye sekta ya kilimo.
Kuanzia mwakani, Bashe amesema Serikali itaanza kugawa bure mbegu za ufuta ambazo zimeshaanza kupandwa na baadhi ya wakulima mkoani Lindi ili kuwaondolea utegemezi wa zao moja la biashara.
Vilevile, maeneo ya Newala ambayo yanafaa kwa kilimo cha soya amesema Serikali itaweka msisitizo kwenye kilimo chake kwa kugawa mbegu za zao hilo kwa wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ili wawe na mazao matatu ya uhakika.
“Huu ndio mwelekeo ili zao moja linapoanguka tunachukua hatua katika zao la pili,” alisema Waziri Bashe.
Katika msimu uliopita, Tanzania ilizalisha tani 240,000 za korosho, huku asilimia 60 ikichangiwa na Mkoa wa Mtwara pekee.
Kwenye msimu huu wa mwaka 2022/23 ambao malengo ni kuzalisha tani 400,000, hadi Novemba 28 taarifa za Bodi ya Korosho Tanzania inasema tani 108,873 zilikuwa zimeuzwa zikiwa na thamani ya Sh209 bilioni. Katika kiasi hicho, Mkoa wa Mtwara ulichangia tani 58,953 zenye thamani ya Sh113 bilioni.
Licha ya kudumu ofisini miezi mitatu mpaka sasa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas anasema kushuka kwa bei na mikorosho mingi kuzeeka ni miongoni mwa changamoto anazoziona kupunguza tija kwa wakulima.
Hali hiyo, anasema sio tu inapunguza kipato cha mkulima mmojammoja hata mapato ya halmashauri kutokana na ushuru unaotozwa.
Kwa miezi hii mitatu naona korosho bado haijainuka sana kwa sababu ya changamoto hizo nilizozisema. Kama kiongozi wa mkoa nina nina dhamana kubwa ya kuhakikisha tunaboresha sekta ya korosho ili iwe na tija kubwa itakayopatikana kwa kuwa na viwanda vya kubangua ilikuachana na usafirishaji wa korosho ghafi kwenda nje ya nchi. nitahakikisha tunakuwa na viwanda hivyo,” anasema Kanali Abbas.
Mkuu huyo wa mkoa amewashauri wakulima kubadilisha mikorosho waliyonayo mashambani kwa kupanda miche mipya iliyofanyiwa utafiti na kuipanda kisasa.
Kupitia jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kituo cha Naliendele, amesema hakuna haja ya wakulima kuendelea kung’ang’ania mbegu za zamani zinazowapa mavuno kidogo, huku wakitumia nguvu kubwa kuhudumia mashamba.
“Korosho ni zao la msimu, hivyo wananchi wa Mtwara wanatakiwa kuwa na shughuli nyingine ya kuwaingizia kipato. Huu ni muda wa mwafaka wa kulima na mazao mengine mbadala ambayo hayategemei msimu kama vile matunda, mbogamboga na vyakula vingine,” ameshauri Kanali Abbas.