Ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia kugusa mambo matano

Waziri Mkuu wa  Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali

Muktasari:

Waziri Mkuu wa  Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa  Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwa na ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini kuanzia Februari 29, 2024 kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema hayo leo Februari 27 jijini Dodoma.

Amesema waziri mkuu huyo atakayepokewa na Rais Samia Machi Mosi, Ikulu jijini Dar es Salaam, anakuja nchini katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya taifa hilo na Tanzania.

Kiongozi huyo ambaye leo yupo nchini Kenya, ziara yake nchini itawezesha kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo, usafiri wa anga, nishati na elimu.

Makamba amesema Tanzania na Ethiopia zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.

“Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao uliasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na mtawala wa Ethiopia,  Haile Selassie.

Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa viongozi waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU mwaka 1963,” amesema.

Waziri Makamba amesema mbali na ushirikiano wa kidiplomasia, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga.

Mwaka 2016 hadi 2023 marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepatiwa mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia.

Ameeleza ziara hiyo itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kujiendesha kibiashara.

Kwenye sekta ya kilimo, Makamba amesema Tanzania na Ethiopia zitaimarisha ushirikiano katika umwagiliaji, matumizi ya teknolojia na mbegu zenye ubora na uhakika wa mavuno na tafiti katika sekta hizo mbili.

“Kuhusu sekta ya nishati, ziara hii itaziwezesha Tanzania na Ethiopia kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika uzalishaji wa umeme unaotosheleza mahitaji ya nchi pamoja na kuzalisha umeme wa kibiashara utakaoiwezesha Tanzania kuuza nje,” amesema.

Kwenye sekta ya elimu, Makamba amesema kupitia ziara hiyo Tanzania na Ethiopia zitabadilishana wanafunzi na kujenga uwezo katika uandaaji wa mitalaa na Tanzania kupata fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia.

Waziri Mkuu Abiy na ujumbe wake wataondoka nchini kurejea Ethiopia Machi 2, 2024.