11 mbaroni wakidaiwa kutapeli, wamo wanawake wawili
Muktasari:
- Jeshi la polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu 11 waliokuwa wameweka kambi jijini Tanga na kuendesha wizi kwa njia ya simu katika mikoa mbalimbali nchini.
Tanga. Jeshi la polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu 11 waliokuwa wameweka kambi jijini Tanga na kuendesha wizi kwa njia ya simu katika mikoa mbalimbali nchini.
Watuhumiwa hao ambao walikuwa wamepanga nyumba katika mtaa wa Donge jijini Tanga na kulipa kodi ya sh 800,000 wamekutwa na simu, line, jiko na chetezo kwa ajili ya kuchomea line na karatasi zenye namba walizolikwishatapeli na wanazotarajia kuendesha utapeli huo pamoja na fedha za Tanzania, Dola za Marekani na fedha za Congo DRC.
Aina ya utapeli waliobainika kuutumia baada ya kuwahoji, Kamanda Mwaibambe amesema walikuwa wakimtaka mwenye simu kutuma fedha na wengine kuomba namba za siri.
Fedha za kitanzania walizokutwa nazo ni Sh2, 085,300, huku za Congo DRC zikiwa ni Faranga 45,100 na dola moja ya kimarekani.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe amewataja waliokamatwa na kuhusishwa na utapeli huo kuwa ni Hadija Nyange (34) mkazi wa Muheza, Zaina Athumani (25) mkazi wa Mwanzange, Mary Mohamed (27) wa Mkanyageni.
Wengine ni Innocent Omeme (35), Abdulaziz Nzori (31), Said Hassan (24), Rashid Habibu (23), Said Juma (30), Idd Kaniki (35), David Rupiana (22), na Salum Rajab (24) wote wakazi wa Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, pia watuhumiwa walikutwa na kadi za simu, pikipiki, kadi za benki, simu ndogo za tochi 13 za aina mbalimbali, na simu janja (smartphone) 11.
"Karatasi tulizowakuta nazo zilikuwa na orodha ya majina ambao waliotapeliwa walikuwa wakiwekewa alama ya tiki na wale ambao ambao hawajatapeliwa waliwekewa alama ya H.
Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kuendesha uhalifu katika mikoa mbalimbali ikiwamo ya kanda ya kaskazini.