155 CCM wautaka ubunge Afrika Mashariki

Muktasari:

Jumla ya wana CCM 155 wameshachukua fomu za kuomba kuwania ubunge wa bunge la Afrika Mashariki.

Dodoma. Jumla ya wana CCM 155 wameshachukua fomu za kuomba kuwania ubunge wa bunge la Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC Oganizesheni wa CCM, Dk Maudline Castico leo Jumanne, Agosti 9, 2022 alipozungumza na waaandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma.

Dk Maudline amesema kuwa, leo katika ofisi za CCM Zanzibar hakukuwa na mwanachama aliyeomba nafasi wakati Ofisi ndogo ya Dar es Salaam walichukua wanachama 16 na Dodoma wamechukua 7 na kufanya jumla ya leo kuwa 23.

Miongoni mwa majina makubwa yaliyochomoza leo Balozi Dk James Msekela ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Tabora Kaskazini na Shyrose Bhanji ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Afrika Mashariki.

Dk Msekela pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na ameshika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwingine ni Juma Ikangaa ambaye ni gwiji wa mchezo wa riadhaa nchini.

Uchukuaji fomu kwa CCM ulifunguliwa Agosti Mosi, 2022 na unatarajia kufungwa kesho Agost 10, 2022.

Nafasi zinazogombewa kwa wabunge kutoka Tanzania ni tisa ambazo mgawanyo wake unaangalia kwa vyama vyenye uwakilishi bungeni hivyo CCM kitakuwa na viti pungufu ya tisa.