20 wauawa shambulio la anga Sudan
Muktasari:
- Watu 20 wameuawa nchini Sudan Kusini Magharibi mji wa Khartoum kufuatia shambulio la anga lililofanywa na jeshi la nchini humo.
Sudan. Shambulio la anga la jeshi katika mji mkuu wa Sudan limeua takriban watu 20, wakiwemo watoto wawili jana Jumapili, wanaharakati wamesema.
Wengi wa waathiriwa wa shambulio hilo, katika kitongoji cha Kalakla al-Qubba kusini magharibi mwa Khartoum, wamezikwa kwenye vifusi, walisema.
Milio ya risasi na roketi imeripotiwa katika maeneo kadhaa nchini humo jana.
Jeshi na wanajeshi wa RSF wamekuwa wakipigania udhibiti wa Khartoum tangu Aprili ambapo hadi sasa mamia ya raia wameuawa.
Wizara ya afya nchini humo imesema zaidi ya watu 1,100 wamefariki nchini humo, lakini idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.
Takriban watu milioni 2.2 wamekimbia makazi yao ndani ya Sudan na zaidi ya nusu milioni wanahifadhiwa katika nchi jirani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Mzozo huo ulianza baada ya mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na mkuu wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kutofautiana kuhusu mustakabali wa nchi.
Mikakati kadhaa ya kusitisha mapigano imetangazwa kuruhusu watu kutoroka mapigano lakini hayajazingatiwa.
RSF inadhibiti sehemu kubwa ya Khartoum na miji yake pacha ya Omdurman na Bahri.
Jeshi limefanya mashambulizi ya mara kwa mara ya mizinga na angani ili kujaribu kuwatimua wapiganaji hao wa kijeshi.
Mapigano yameenea nje ya mji mkuu, ikiwa ni pamoja na eneo la magharibi la Darfur ambalo limeshuhudia kuzuka kwa ghasia za kikabila.