206 wafutiwa matokeo kidato cha pili, darasa la nne

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (Necta), Dk Said Mohammed akitangaza matokeo ya mitihani darasa la nne na kidato cha pili mwaka 2023 jijini Dar es salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya upimaji darasa la nne na kidato cha pili huku ufaulu wa somo la hesabu ukiendelea kuwa chini.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kitaifa ya upimaji wa darasa la nne na kidato cha pili uliofanyika mwaka 2023 ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.13 kwa kidato cha pili na asilimia 0.39 kwa darasa la nne.

Katika matokeo ya darasa la nne, taarifa inaonyesha wanafunzi 1,287,934 sawa na asilimia 83.34 wamefaulu kuendelea na darasa la tano.

Upande wa kidato cha pili, wanafunzi 592,741 ambao ni sawa na asilimia 85.31 wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la nne.

Akitangaza matokeo hayo leo Jumapili, Januari 7, 2024 Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed amesema baraza hilo pia limefuta matokeo kwa wanafunzi 178 wa darasa la nne na 28 wa kidato cha pili waliofanya udanganyifu.

Mbali na hao, baraza limewafutia matokeo wanafunzi watatu wa darasa la nne na 14 wa kidato cha pili walioandika matusi.

Kwa upande wa masomo kwa darasa la nne, matokeo hayo yanaonyesha ufaulu wa sayansi na teknolojia ukifikia asilimia 86.86 kutoka asilimia 83.19 ya mwaka 2022 na somo la hisabati likifiki asilimia 54.00 kutoka asilimia 49.7.

Kwa kidato cha pili, ufaulu wa somo la uraia umeimarika kutoka asilimia 31.12 mwaka 2022 hadi kufiki asilimia 48.27.