Matokeo kidato cha nne gumzo
Dar/Dodoma. Siku moja tangu Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) litangaze matokeo yamtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2022, mijadala imeendelea kutawala juu ya sintofahamu zilizomo, huku Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikisisitiza msimamo wa Necta wa kutokutangaza shule wala wanafunzi bora.
Matokeo ya mitihani hiyo iliyofanyika kati ya Novemba 14 hadi Desemba 1 mwaka jana, yalitangazwa juzi huku Necta ikikazia utaratibu mpya iliouanza wakati ikitangaza matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili kuwa kubainisha shule na wanafunzi waliofanya vizuri hakuna tija, bali ni kuzingaza tu shule na kuwapima waliosoma katika mazingira tofauti.
Mbali na hilo na matokeo mbaya katika shule nyingi, matukio ya matokeo ya mvulana kuonekana katika shule ya wasichana pamoja na yale ya mwanafunzi mmoja kutolewa huku wenzake wote 66 wakiwa wamefutiwa udanganyifu ni mambo yaliyozua mjadala.
Matokeo ya shule ya wasichana ya Musabe ya jijini Mwanza yameibua maswali wadau wakihoji inawezekanaje shule yenye wasichana pekee, tena ya bweni, awepo mvulana aliyefanya mtihani?
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema hayo ni matatizo ya usajili lakini mwanafunzi huyo si mvulana bali ni msichana.
“Ni matatizo ya usajili, jina na jinsi zitabadilishwa (kwenye matokeo,” Hata hivyo, hadi jana saa 12 jioni vilikuwa havijabadilishwa.
Suala jingine lililoibua sintofahamu ni matokeo Shule ya Sekondari Twibhoki ya mkoani Mara ambayo ilikuwa na wanafunzi 67 waliofanya mitihani, lakini matiokeo yaliyotoka ni mmoja tu mwenye namba S5253/0034 ndiye matokeo yake yametolewa na wengine wote kuwekewa (---).
Mwanafunzi huyo amepata daraja la kwanza akiwa na alama nane.
Gazeti hili lilipotaka kujua nini kimetokea kwa shule hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Amas alisema matokeo ya shule hiyo yamefutwa kutokana na vitendo vya udanganyifu.
“Wamejihusisha na udanganyifu, mwanafunzi ambaye hakuhusika na udanganyifu hakufutiwa matokeo yake,” alisema.
Aidha, katika matokeo hayo kwa ujumla, Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 333 wakiwemo wanne walioandika matusi kwenye karatasi zao za majibu.
Alipoulizwa juu ya hatua zinazochukuliwa kwa wanafunzi wanaobainika kuandika matusi kwenye mitihani, Amasi alisema hatua pekee inayochukuliwa ni kufuta matokeo.
Katika hilo, Mwanasaikolojia Charles Mhando alisema wanafunzi kuandika matusi kwenye mitihani kunasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kutojiandaa vyema kabla ya mitihani.
“Hiyo pia ni ishara ya kuwa mwanafunzi husika hafahamu umuhimu wa elimu katika maisha yake na ndio maana haingiwi na hofu ya kufanya vitendo vitakavyoiweka rehani elimu yake,” alisema.
Kauli ya wizara ya elimu
Kufuatia mijadala ya ama kutangaza au kutokutangaza shule na wanafunzi bora, gazeti hili lilimtafuta, Kamisha wa Elimu nchini, Dk Lyabwene Mtahabwa aliyesema, “msimamo wa Necta ndiyo msimamo wa wizara ya elimu.”
Alichokisema Dk Mtahabwa kilifafanuliwa pia na Amasi kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kugundulika baadhi ya shule kujiingiza kwenye michezo michafu ili zitangazwe shule bora zinufaike kibiashara.
“Utaratibu huo umebadilika kutokana na baadhi ya watu kuhamasika kutaka kuwa wa kwanza, walikuwa wanaiba ili waongoze,” alisema.
‘Ni wazo bovu’
Hoja ya kutokutangaza wanafunzi au shule limezungumziwa pia na Profesa Thadeus Mkamwa, mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine, tawi la Mtwara kuwa kutotangaza waliofanya vizuri huenda ni nadharia nzuri ya kuwanyenyekesha washindi kwa kuwanyima haki yao ya kufurahia ‘perfomance’ (mafanikio) yao.
“Ni wazo bovu kiuhalisia kwa sababu kudai kwamba ukimtangaza aliyeshinda kuliko wote ni kumpigia debe ni kujidanganya.
“Wa kwanza ni wa kwanza tu hata umuite wa mwisho na debe amejipigia mwenyewe kwa performance. Wewe mtangazaji unatangaza tu huongezi wala hupunguzi huo ushindi,” alisema Profesa Mkamwa.
Profesa Mkamwa ambaye ni padri wa Kanisa Katoliki alitoa wito kwa shule zinazofanya vizuri zisikatishwe tamaa kwa kufunikwa katika blanketi la nadharia ambayo haina tija katika nyanja mbalimbali.
“Sasa, hofu ya nini kushindwa kuwaheshimisha Tanzania One kama desturi? Kwangu mimi naona wamekosewa, jambo kubwa katika maendeleo yao ya kielimu katika uchanga wao. Tujenge elimu katika ukweli na uwazi,” alihitimisha.
Wabunge washangazwa
Profesa Kitila Mkumbo (Ubungo) na Nusrat Hanje wa Viti Maalumu nao waonyesha kutokukubaliana na uamuzi huo wa Necta.
Mulugo aliyewahi kuwa naibu waziri wa elimu na mmiliki wa shule alisema hakutarajia kama jambo hilo lingeweza kutokea katika kipindi ambacho Serikali inajaribu kufundisha kwa jitihada ili kuongeza ushindani kwenye shule za msingi na sekondari.
“Unapofanya hivyo kama Serikali unataka kusiwe na mwanafunzi wa kwanza hadi wa mwisho, lazima itokee tu hata kwa Mungu ipo,” alisema Mulugo.
Alisema kama wadau wa elimu anaona kama ni sehemu ya kuficha mabaya, yaani wanafunzi wanapofeli sana ndio wanaanza kuficha, jambo hilo ni hatari sana kwa Taifa.
“Hii ni kama Simba na Yanga, maana ukitaka kutangaza ushindi ni kuwa unawatangazia biashara? Hapana wamefanya vizuri ndiyo maana wanafunga magoli,” alisema.
Naye Profesa Mkumbo alisema miongoni mwa faida za kuzipanga shule kwa kuzingatia kiwango cha kufaulu ni kuchochea shule kuweka mazingira mazuri ya walimu na wanafunzi kusoma kwa bidi zaidi ili waendelee kufanya vizuri zaidi.
“Hasara mojawapo ya utaratibu huu ni uwezekano wa kuzisukuma baadhi ya shule zijikite zaidi katika kuwezesha wanafunzi kufaulu mitihani badala ya kujikita katika kujifunza wapate maarifa na stadi,” alisema Profesa Kitila aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, alisema upangaji wa shule na wanafunzi kwa kuzingatia kiwango cha ufaulu unaweza kuleta athari za kuwatia unyonge baadhi ya wanafunzi na hivyo kushusha ari na motisha wa kujifunzia.
Hata hivyo, alisema kwa ujumla, wake tafiti zinaonyesha hakuna athari kubwa (hasi au chanya) inayotokana na utaratibu wa kupanga shule kitaaluma.
Alisema utaratibu wa kupanga shule umeshazoeleka sana miongoni mwa wazazi na jamii nchini na umekuwa ukitumika kuwasaidia wazazi kuchagua shule za kuwapeleka watoto, ingefaa uruhusiwe kuendelea lakini kwa kufanya maboresho.
Aidha, alisema nchi jirani ya Kenya waliwahi kupiga marufuku utaratibu huo mwaka 2014 kwa kigezo kuwa ulikuwa unachochea wizi wa mitihani lakini hata hivyo wizi wa mitihani haukukoma na ikaja kuonekana wizi ulikuwa hausababishwi na utaratibu huo pekee.
Alisema kutokana na msukumo wa mkubwa wa wazazi na umma Serikali ililazimika kuurejesha utaratibu mwaka 2016 lakini ukiwa umeboreshwa.
Hanje ambaye kitaalama ni mwalimu alisema ni sahihi kuondoa mfumo huo wa upangaji wa matokeo kwa sababu haukuwa halisia wa mazingira unaofanana kwa kitu chochote.
Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Mariam Mbwana (Dar) na Sharon Sauwa (Dodoma).