Matokeo kidato cha nne yatangazwa, 333 yafutwa na wanne waandika matusi

Muktasari:

Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 14 hadi Desemba 1, 2022, Tanzania Bara na Visiwani huku likiwafutia wanafunzi 333 kwa udanganyifu.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 14 hadi Desemba 1, 2022, Tanzania Bara na Visiwani huku likiwafutia wanafunzi 333 kwa udanganyifu.

Akizungumza leo Jumapili, Januari 29, 2023, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi amesema kati ya watahiniwa hao mmoja ni wa maarifa (QT) na 332 watahiniwa wa shule.

"Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 333 kwa kufanya udanganyifu, kati yao mmoja ni mtahiniwa wa maarifa na 332 ni wa shule," amesema.

Ametaja watahiniwa wengine waliofutiwa matokeo ni wanne ambao wameandika matusi katika mitihani yao.

Kwa mujibu wa Amasi, vituo vitatu vimefungiwa kufanya mitihani baada ya kuthibitika kupanga na kufanya udanganyifu.

Amevitaja vituo hivyo ni Andrew Faza Memorial cha Kinondoni Dar es Salaam, Cornelius cha Kinondoni na Mnemonic Academy cha Halmashauri ya Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Katika matokeo hayo, Amasi amesema kati ya watahiniwa 520,558 wenye matokeo 456,975 sawa na asilimia 87.79 wamefaulu kwa kupata madaraja ya kwanza hadi la nne.

Ameeleza ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 0.49 kutoka wa mwaka jana ambapo watahiniwa 422,388 sawa na asilimia 87.30 walifaulu.