23 kutoa ushahidi kesi ya mume, mke wanaodaiwa kusafirisha unga
Mshtakiwa Najim Mohamed (aliyevaa barakoa) akiwa na Juma Abbas wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 3050 za Heroine na Methamphetamine, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Najim, mkewe pamoja na mfanyakazi wa ndani wa kiume, wanadaiwa kusafirisha heroini yenye uzito wa kilo 882.71, pamoja na methamphetamine yenye uzito wa kilo 2167.29, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba 15, 2023 eneo la Kibugumo Shule, wilayani Kigamboni.
Dar es Salaam. Mashahidi 23 na vielelezo 62 wanatarajia kutoa ushahidi wao mahakamani katika kesi ya kusafirisha shehena ya kilo 3,050 za dawa za kulevya aina ya heroini na methamphetamine, inayomkabili mfanyabiashara Najim Mohamed (52) na mkewe Maryam Najim Mohamedi (50) pamoja na mfanyakazi wa ndani, Juma Abbas (37).
Dawa hizo zinadaiwa zilikuwa zimehifadhiwa katika kontena za plastiki 1478 pamoja na pakiti 824 nyumbani kwa mshtakiwa Najim, eneo la Kibugumo Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali, Edith Msenga akishirikiana na Erick Davies ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mwisho mwa wiki iliyopita, wakati wakiwasomea idadi ya mashahidi na vielelezo pamoja na maelezo ya mashahidi.
Mohamed na wenzake anakabiliwa na kesi ya uhujumu namba 41113 ya mwaka 2023 yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 882.71 na methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, pindi kesi hiyo itakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Mshtakiwa Maryam Mohamed anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya pamoja na mume wake Najim Mohamed pamoja na mfanyakazi wa ndani wa kiume Juma Abbas, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Washtakiwa hao ambao wanatetewa na wakili Taher Muccadam, wamesomewa maelezo ya mashahidi na vielekezo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Jamhuri baada ya kutoa taarifa hiyo iliwasomea upya mashtaka yao na kisha maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Wakili Msenga alidai kati ya mashahidi 23 watakaotoa ushahidi mahakamani, wapo maofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA), wapelelezi wake, maofisa kutoka Jeshi la Polisi pamoja na wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Pia ilidaiwa mahakamani hapo kati ya vielelezo hivyo 62; nyaraka halisi ni 40 na nyaraka za vielelezo ni 22.
Wakili Msenga alidai katika nyaraka halisi (40) kuna ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali, leseni mbili za umiliki silaha aina ya bastola baretta na shotgun double barrel zenye jina la Najim, hati ya ukamataji, hati ya upekuzi, maelezo ya onyo ya mshtakiwa Najim, ripoti ya uchunguzi kutoka Cyber, barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kitambulisho cha Taifa (Nida) na hati ya kusafiria ya mshtakiwa Najim.
Pia, nyaraka zingine ni za umiliki wa magari matano, kadi ya mbili za benki ya CRDB na Amana zenye jina la Najim na kadi moja ya benki ya Amana MasterCard yenye jina la Maryam.
Vilevile katika nyaraka za vielelezo (22), wakili Davies alivitaja ni kilo 882.71 za heroini, kontena 1,478 za plastiki zenye dawa za kulevya, pakiti 824 zenye dawa za kulevya aina ya heroini, mabegi mawili ya nguo na mfuko mmoja wa salifeti.
Vingine ni dola za marekani USD 10,000, fedha ya Uganda Sh110,000, fedha ya Kenya Sh6,500 na fedha ya Tanzania Sh10 milioni pamoja na magari matatu aina ya Toyota Hilux na Nissan Patrol na funguo zake.
Mshtakiwa Najim Mohamed (aliyevaa barakoa) akiwa na Juma Abbas wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 3050 za Heroine na Methamphetamine, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo. Picha na Hadija Jumanne
Vielelezo vingine ni simu tano zikiwemo Iphone mbili na Samsung Galax tatu, mifuko ya salfeti 153, ambayo 125 ilikuwa imewekewa kontena la plastiki zenye dawa za kulevya na 28 haikuwa na kitu.
Pia, kuna flash 30 zenye picha za dawa za kulevya aina ya methamphetamine, silaha mbili aina ya bastola Baretta na shotgun double barrel, sampuli tano za mwandiko zilizowekwa alama pamoja na flashi moja ya iliyohifadhi mawasiliano ya simu za washtakiwa hao.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya aliwaambia washtakiwa hao kesi yao ameihamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji. Hivyo wakati wakisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashitaka washtakiwa hao watakuwa rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 29, 2023 na kusomewa kesi hiyo, ambayo hawakutakiwa kujibu chochote.