Raia wa Kenya akutwa na kesi ya kujibu

Raia wa Kenya, Josephine Mumbi Waithera (aliyejifunika), akiwa chini ya ulinzi katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Picha na Daniel Mjema
Muktasari:
Mwaka 2016, raia huyo wa Kenya, Josephine Mumbi Waithera alihukumiwa kifungo cha maisha.
Moshi. Mahakama Kuu kanda ya Moshi imemuona raia wa Kenya, Josephine Mumbi Waithera kuwa ana kesi ya kujibu katika shitaka la kusafirisha dawa za kulevya kwenda Vienna nchini Austria.
Uamuzi huo ulitolewa leo Julai 31,2018 na Jaji Patricia Fikirini baada ya upande wa mashtaka katika kesi hiyo, kufunga ushahidi wao wakimalizia na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi.
Ng’anzi ambaye ni Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), ndiye aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya Jinai (RCO) mkoa Kilimanjaro wakati mtuhumiwa huyo anakamatwa 2012.
Soma Zaidi:
Katika uamuzi wake huo, Jaji Fikirini amesema kutokana na ushahidi wa mashahidi sita na vielelezo nane vya upande wa mashitaka, amemuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu hivyo atatakiwa kujitetea.
Mshitakiwa huyo ataanza kujitetea leo saa 8:00 mchana.
Mwaka 2016, raia huyo wa Kenya, Josephine Mumbi Waithera alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia katika kosa hilo, lakini Mahakama ya Rufaa ikaamuru kesi isikilizwe upya.
Hukumu ya awali ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari, lakini mwaka jana Mahakama ya rufani ikaamuru isikilizwe upya baada ya kubaini dosari za kisheria.
Josephine alikamatwa Juni 4, 2012 katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Kilimanjaro (KIA), akituhumiwa kusafirisha gramu 3,249 za dawa za kulevya aina ya Heroin kwenye Vienna, Austria.
Dawa hizo zinazodaiwa kuwa na thamani ya Sh146.2 milioni, zinadaiwa kuhifadhiwa katika begi kubwa, zikiwa zimefungwa katika plastic ngumu na baadae kuwekwa katika mfuko wa nailoni.