Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi mjitafakari maadili ya watoto

Muktasari:

  • Lengo si tu kuujaza ulimwengu bali kuhakikisha tunarithisha maadili mema kwa watoto wetu.

Dar es Salaam. Katika hali ya sasa, ni wazi kuwa wazazi wengi wamekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwa watoto wao.

Nasema hivi kwa sababu ingawa binadamu tunaendelea kuzaa na kuongeza kizazi, lengo si tu kuujaza ulimwengu bali kuhakikisha tunarithisha maadili mema kwa watoto wetu.

Vitabu vitakatifu vimekuwa vikikazia wajibu huu muhimu wa wazazi ni pamoja na kulea sambamba na kuwafundisha watoto maadili ili nao wawarithishe watoto wao wakiwa na familia zao.

Ndiyo maana wazazi na walezi wanapaswa kuwalea watoto kwa umakini, kuhakikisha wanatambua mema na mabaya wakiwa bado wadogo. Methali ya "mtoto ni kama samaki, akikauka hakunjiki" inaeleza vyema hili.

Kwa mfano, katika biashara ya samaki wakavu, ili usafirishaji uwe rahisi, samaki hukunjwa akiwa mbichi. Lakini sasa, wazazi wengi wanajaribu kuwakunja watoto wao wakiwa tayari ‘wamekauka’ jambo lisilowezekana.

Hali hii imechangia kilio cha kuporomoka kwa maadili kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kiongezeke kila uchao.

Ni kweli kuna ongezeko la vitendo vya aibu na vya kuhatarisha jamii kama wizi, ulawiti, ubakaji, mapenzi ya jinsia moja, ujambazi, mauaji, uvaaji usio na heshima, matumizi ya dawa za kulevya na pombe kupita kiasi.

Ukiangalia kwa kina, tatizo hili lina mizizi kwenye mifumo ya malezi na hata elimu. Watoto wanaachwa wakiishi kwa njia inayofedhehesha bila hatua madhubuti kuchukuliwa pale wanapoanza kuharibika kimaadili.

Msingi wa malezi bora unaanzia nyumbani kwa baba na mama. Kwa mfano tutategemeaje mtoto awe na hofu ya Mungu kama wazazi wenyewe hawashiriki ibada kanisani au msikitini? Mtoto atajengewaje wazo la dhambi kama hajui uwepo wa Mungu?

Wazazi au walezi wana wajibu mkubwa wa kutengeneza msingi wa kimaadili kwa mtoto tangu akiwa mdogo, kumfundisha kutofautisha mema na mabaya.

Bila umakini, watoto wetu hawatabaki salama hasa katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya teknolojia. Teknolojia inapaswa kutumika kwa manufaa, si kama chombo cha kupotosha watoto na jamii.

Kwa mfano, ni jambo linalotia shaka kuona wazazi wakiwapa watoto uhuru usio na mipaka kuangalia vipindi vyote kwenye televisheni hata vile vyenye maudhui yasiyofaa kimaadili.

Wazazi tunapenda watoto watazame katuni, lakini je tunakagua kama vipindi hivyo vinafundisha maadili mema au vinaharibu?

Kuna katuni, vitabu na filamu zinazochochea tabia za mapenzi ya jinsia moja na mambo mengine yasiyofaa.

Wazazi wengi wanakaa kimya wakitazama watoto wakiharibika kimaadili na kuwa mzigo kwa jamii.

Tumeanza kuyakubali matukio haya kana kwamba ni mambo ya kawaida wakati ni msiba wa kimaadili kwa familia na jamii.

Niliwahi kusoma ripoti ya Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) inayoonyesha asilimia 57 ya Watanzania hawako kwenye ndoa, jambo linalotajwa kama moja ya sababu za watoto kukosa malezi bora na hivyo kuporomoka kwa maadili.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa vijana wengi nchini hawana maadili wala stadi za maisha. Utafiti huo ulihusisha watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 katika wilaya 34, kaya 11,802 na vijana 14,645.

Utafiti ulipima uwezo wa mtoto kwenye maadili na stadi za maisha, ikiwamo uwezo wa kutatua matatizo, kujitambua, heshima kwa wengine na ushirikiano.

Lakini matokeo yanaonesha asilimia 7.6 pekee wanaweza kutatua matatizo yao, asilimia 16.8 wanajielewa na wana njia nyingi za kufikia malengo.

Lakini pia inaonyesha vijana wenye heshima kwa wengine kwa kiwango cha juu ni asilimia 12.5, wanaoshirikiana na wengine kwa kiasi kikubwa ni asilimia 11.4.

Kwa ujumla, ni asilimia 12 tu ya vijana wenye maadili na stadi za maisha bora ni sawa na mmoja kati ya 10.

Huu ni ujumbe wa wazi kwa wazazi, msiishie tu kufuatilia matokeo ya mitihani shuleni, bali hakikisheni mnamfundisha mtoto maadili na stadi za maisha.

Mzazi lazima ujitathmini na kujiuliza unamleaje mtoto wako? Anaweza kuwa na akili kubwa ya kufaulu darasani, lakini kama hajalelewa kimaadili hiyo ni kazi bure.

Tunalia kila siku kuhusu kushuka kwa maadili ya vijana, lakini chanzo chake ni mitindo ya maisha inayoanzia kwenye familia.

Umri wa vijana waliohojiwa kwenye utafiti huo unaonyesha wazi kwamba wazazi na jamii wana mchango mkubwa kwenye hili.

Hata ukifanya utafiti kuhusu maadili, utapata majibu yanayofanana na ripoti hii inaweka wazi hilo.

Pia, ongezeko la malezi ya mzazi mmoja limechangia kuporomoka kwa maadili.

Wazazi wanalo jukumu kubwa. Siku hizi, watoto wadogo wanamiliki simu na wanaiga mambo ambayo si sehemu ya utamaduni wetu.

Hivyo wazazi mna kazi kubwa mbele yenu. Msitarajie walimu shuleni wawafundishe watoto wenu maadili tu. Ni jukumu lenu kuhakikisha kizazi hiki kinalelewa vizuri na hakiteketei kimaadili.