25 waliofariki kwa ajali Arusha kuagwa kesho
Muktasari:
- Ajali iliyokatisha uhai wa watu 25 na kujeruhi 21 ilitokea Jumamosi Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni) katika Barabara Kuu ya Arusha – Namanga.
Arusha. Serikali kesho wataiaga miili ya watu waliofariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea juzi eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), Barabara Kuu ya Arusha-Namanga.
Ajali iliyotokea Jumamosi ya Februari 24, 2024 ikihusisha lori mali ya Kampuni ya KAY Construction ya Nairobi, Kenya na magari mengine madogo matatu, ilisababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi wengine 21.
Majeruhi bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na Selian.
Magari mengine yaliyopata ajali katika tukio hilo ni T 623 CQF aina ya Nissan Caravan, T 879 DBY aina ya Mercedes Benz Saloon na T 673 DEW aina ya Toyota Coaster mali ya shule ya mchepuo wa Kingereza ya New Vision.
Chanzo cha ajali kinaelezwa kuwa ni kufeli kwa mfumo wa breki wa lori na kwenda kuyagonga magari hayo mengine yaliyokuwa mbele yake.
Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji alisema jana kuwa, winaendelea kumsaka dereva wa lori hilo anayedaiwa kutoroka baada ya ajali.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Februari 26, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema miili hiyo itaagwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Amesema Serikali imeahidi kutoa mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila mwili.
Wakati huohuo, mkuu huyo wa mkoa amesema wananchi wataanza kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa tatu asubuhi.
“Kuanzia saa tatu asubuhi tutaanza zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa miili ya hawa ndugu zetu tunaoenda kuwapumzisha," amesema Mongela.
Hata hivyo, Mongela amesema kabla ya kuanza kuaga miili hiyo, kutakuwa na ibada maalumu itakayofanyika.
Mpaka leo saa saba mchana, idadi ya vifo ni 25 na majeruhi 21.