250 wajiandikisha kufanya upasuaji kurekebisha maumbile Tanga
Baadhi ya wananchi waliofika Hospital ya Rufaa ya Bombo kwaajili ya kupatiwa huduma ya kurekebisha maumbile
Muktasari:
- Madaktari bingwa 14 kutoka Ujerumani wamesili mkoani Tanga kufanya huduma za kurekebishamMaumbile (plastic Surgery).
Tanga. Uchunguzi wa awali wa watu zaidi ya watu 250 waliojiandikisha kwa ajili ya huduma za kibingwa za kurekebisha maumbile (plastic surgery) umeanza leo Julai 14, 2023 katika Hospitaliya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.
Huduma hiyo ya kurekebisha maumbile inafanywa na madaktari bingwa 14 kutoka Ujerumani.
Akizungumza baada ya madaktari hao kuwasili, mratibu wa kambi ya upasuaji wa kurekebisha maumbile katika hospitali hiyo, Dk Wallace Karata amesema baada ya kuwasili hospitalini hapo, wameanza kufanya uchunguzi wa awali na baadae kupangiwa ratiba kwa ajili ya upasuaji.
Dk Karata aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito ambapo zaidi ya wagonjwa 250 wamejiandikisha na wataonwa leo na kesho kwa ajili ya kupangiwa siku ya zoezi la upasuaji.
“Madaktari hao wanakuja kutoa huduma kwa watanzania ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu za upasuaji na kurekebisha maumbile, hawa wameamua kuja kutoa bure kama msaada kwa watanzania,” amesema Dk Karata.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji katika hospitali hiyo, Dk Rashid Suleiman amesema madaktari hao wamekuja kufuatia ushirikiano mbao umedumu kwa miaka 13 tangu ulipoanza.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Naima Yusuf ameshukuru kwa matayarisho yaliyofanyika ikiwemo kuungwa mkono na uongozi kuanzia ngazi ya wizara kupitia kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Amewahakikishia wote waliosajiliwa kuwa watafanyiwa uchunguzi kisha watafanyiwa upasuaji kuanzi kesho Julai 15, 2023 hadi Julai 28, 2023.
Baadhi ya wananchi wa Jiji la Tanga wamesema huduma hiyo itawasaidia kurekebisha maumbile yao.