Huduma ya kuwekewa puto sasa kupatikana Arusha, Mwanza

Daktari bingwa wa upasuaji na mtaalamu wa Endoscopia, Erick Muhumba akiongoza jopo la wataalamu kumwekea puto mmoja wa wagonjwa waliojitokeza kwa ajili hiyo. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Ikiwa imepita miezi michache tangu Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam kuzindua huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito uliopitiliza (intragastic ballon), huduma hiyo sasa imesogezwa katika Mkoa wa Mwanza.

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi michache tangu Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam kuzindua huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito uliopitiliza (intragastic ballon), huduma hiyo sasa imesogezwa  katika Mkoa wa Mwanza.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Mach 7, 2023 na Magreth Mashobe ambaye ni Meneja Masoko wa Plastic Surgery Coordinators Tanzania ambao ni waratibu wa masuala ya urembo au marekebisho mbalimbali ya mwili katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mashobe amesema huduma hiyo kwa Mkoa wa Mwanza itakuwa ikitolewa katika Hospitali ya CF na jijini Arusha itatolewa katika Hospitali ya Seliani.

"Pia hata katika Jiji la Dar es Salaam Hospitali ya Seifee nayo itakuwa ikitoa huduma hiyo na tutaendelea kutoa taarifa kadri mikoa mingine inayoendeleya kusogezewa huduma hiyo kwani tangu kuanza kutolewa uhitaji wake unaongezeka kila siku," amesema.

Amesema wanaendelea kusogeza huduma hiyo katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha wahitaji wanaipata kwa ukaribu na kuwaepushia usumbufu na kuwapunguzia gharama.

"Tumeendelea kuhakikisha huduma hii inapatikana sehemu zaidi ndani ya Tanzania ili kuruhusu ushindani wa bei ambao utawapa unafuu wahitaji wa huduma hiyo," amesema.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Saifee Hospitali, Dk Hussein Khanbai ametoa wito kwa Watanzania kuwa na imani na huduma mpya ambazo awali na sasa zilikuwa zinapatikana nje ya nchi na sasa zinapatikana nchini.