Kwa Sh4 milioni unakata kitambi, nyama uzembe

Daktari bingwa wa upasuaji na mtaalamu wa Endoscopia, Erick Muhumba akiongoza jopo la wataalamu kumwekea puto mmoja wa wagonjwa waliojitokeza kwa ajili hiyo. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Aina hii ya tiba ilianza kupata umaarufu nchini mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kuibuka kwa majibizano kwenye mitandao ya kijamii baina ya wafanyabiashara wawili baada ya mmoja kumshutumu mwenzake kuwa anadanganya umma kuwa amepungua kutokana na dawa za kupunguza uzito wakati ukweli ni kwamba amewekewa puto nje ya nchi.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watu wakijinyima kula, kutumia dawa za asili, za kisasa na kufanya mazoezi ili kupunguza vitambi na uzito, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Mloganzila) imekuja na njia salama ya kuwawekea puto tumboni wenye matatizo hayo kwa Sh4.2 milioni.
Tayari watu wameanza kuchangamkia fursa hiyo na taarifa kutoka Mloganzila zinaeleza kuwa hadi Jumatano iliyopita watu 27 wameshawekewa puto hili, akiwamo mwanamuziki Peter Msechu, aliyepatiwa tiba hiyo Januari 25.

Tiba hiyo ya kuweka puto kwenye tumbo la chakula inaelezwa kuwa bora na yenye matokeo ya haraka zaidi ikilinganishwa na nyingine kama kukata utumbo na aina nyingine za upasuaji zenye lengo la kupunguza uzito.

Tatizo ni kubwa
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya watu wenye uzito kupita kiasi inaongezeka nchini, waathirika wakubwa wakiwa wanawake.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wana uzito uliopitiliza.

Hali hii imekuwa ikiwakosesha raha wengi na kujikuta wakitafuta njia mbalimbali za kupunguza uzito za asili na za kitaalamu.


Tiba yenyewe
Aina hii ya tiba ilianza kupata umaarufu nchini mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kuibuka kwa majibizano kwenye mitandao ya kijamii baina ya wafanyabiashara wawili baada ya mmoja kumshutumu mwenzake kuwa anadanganya umma kuwa amepungua kutokana na dawa za kupunguza uzito wakati ukweli ni kwamba amewekewa puto nje ya nchi.

Hilo liliwafanya wengi watake kujua kuhusu puto hilo linaloelezwa kusaidia kupunguza unene kwa haraka.

Huduma hiyo ya kibingwa inayofahamika kama ‘intra-gastric balloon’ awali ilikuwa ikipatikana katika mataifa yaliyopiga hatua katika upasuaji wa kurekebisha viungo kama vile Uturuki na Afrika Kusini.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, daktari bingwa wa upasuaji na mtaalamu wa Endoscopia, Erick Muhumba alisema uwekaji wa puto kwenye tumbo la chakula wenye uzito mkubwa ni moja ya matibabu ya kuwasaidia wenye uzito mkubwa.

“Kwa kiasi kikubwa watu hawa ni wale ambao wanaweza kuwa hatarini kupata au tayari wameshapata magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na unene na uzito mkubwa hivyo kuwasaidia kupungua.

“Hii ni aina ya tiba ambayo ikiwa una uzito kupita kiasi na una matatizo mengine kama vile kisukari cha aina ya pili, shinikizo la damu, changamoto ya upumuaji wakati wa usingizi, matatizo ya kupumua au ugonjwa wa moyo,” alisema.

Dk Muhumba alisema tiba hiyo inasaidia kupunguza nafasi kwenye tumbo la chakula hivyo kumfanya mtu ale kidogo hivyo kupungua uzito.

Alisema kabla ya kuwekwa puto, hufanyika vipimo kujua hali ya afya ya mgonjwa, hususan usalama wa tumbo, shinikizo la damu na vipimo vingine muhimu kwa mujibu wa mapendekezo ya jopo la madaktari.

“Mgonjwa anapofika kwa ajili ya matibabu haya anaonwa na jopo la wataalamu ambalo linaundwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, usingizi na ganzi, upasuaji, maabara na wauguzi.

Endapo vipimo vitabaini mgonjwa kuwa na tatizo lolote, ikiwamo vidonda vya tumbo, mikwaruzo au majeraha hawezi kuwekewa puto hadi atakapopata matibabu na kupona kabisa.

“Kitu cha kwanza baada ya vipimo vya kawaida huwa tunaangalia tumbo kama lipo sawa, hili hufanyika mgonjwa akiwa tayari amelazwa kwa dawa za usingizi. Tumbo likiwa sawa tunaingiza puto kupitia mdomoni kwenda kwenye utumbo wa chakula.

“Puto likishakaa kwenye utumbo yanawekwa maji ya rangi ambayo mara nyingi tunaweka kati ya mililita 350 hadi 550, lakini ukubwa wa puto lenyewe unaweza kuchukua mililita 800. Kazi hii hufanyika ndani ya dakika 30 hivyo mgonjwa anaweza kuamka na kuendelea na shughuli zake baada ya saa moja,” Dk Muhumba.


Kuishi na puto
“Ukiwa na puto tumboni utakula kiasi kidogo cha chakula, kwa maana utumbo utazoea kupata kitu kidogo na kipindi hicho unapaswa kuendelea kuzingatia mazoezi na mlo kamili,” alisema.

Dk Kitembo Kibwana alisema endapo aliyewekewa puto atazingatia masharti, puto litakapotolewa hataongezeka uzito.

“Ukiendelea kula kidogo hutaongezeka uzito kwa kasi kwa kuwa utakuwa umeshajitengenezea mfumo mzuri, lakini ukienda kinyume utapata matokeo tofauti,” alisema.

Daktari huyo alisema kuna aina za maputo; yanayoweza kukaa tumboni miezi sita, tisa na mwaka mmoja.

“Kwa sasa tunatumia yanayokaa mwaka mmoja na usalama wake ni mkubwa, haya ni American gastric balloon, kwa wanaojua tiba hii, hizi ndizo balloon za kisasa zaidi na zenye ubora. Muhimu ni kuboresha mwenendo wako wa ulaji ili uweze kupunguza uzito hata pale puto litakapoondolewa,” anasema Dk Kitembo.

Kuhusu gharama, Dk Muhumba alisema tiba ya puto ni kati ya Sh4.2 milioni na Sh4.5 milioni.

“Tofauti hii ndogo ya gharama hutokana na aina ya vipimo ambavyo daktari ameona vinahitajika kwa mgonjwa husika.

Hata hivyo, huduma kama hii Afrika Kusini inatolewa kwa Sh16 milioni, hivi karibuni tumemfanyia raia wa Afrika Kusini na si huyo tu, watu wengi wa nchi jirani wameonyesha nia ya kufuata matibabu hapa Mloganzila,” alisema.


Kisa cha Msechu
Akizungumza muda mfupi kabla ya kupatiwa tiba hiyo, Msechu alisema aliamua kufanya hivyo kwa sababu alikuwa amechoshwa na maneno aliyokuwa akiambiwa au kusoma mitandaoni.

“Watu wananisema sana mitandaoni kuhusu unene wangu lakini siwajibu, niliamua kuishi maisha yangu. Pamoja na hali hiyo nimekuwa kila siku nikitafuta tiba mbadala ya kuondoa unene kwa kuwa natamani sana kupungua.

“Changamoto ya unene unakuwa mtu wa kuchagua vitu, wakati mwingine nahofia kuvunja vitanda vya hoteli kwa sababu nilishavunja sana, hasa chaga.”

Ndani ya dakika 40 kazi ya kuweka puto hilo kwenye tumbo la Msechu ilikamilika na akaendelea na shughuli zake.
“Hakuna maumivu yoyote niliyosikia, nilipewa dawa za usingizi, nilionyeshwa tu video kwamba puto limeshawekwa. Naamini hii itakuwa suluhisho kwa tatizo langu maana nimehangaika kwa muda mrefu kutumia dawa, hakuna aina yoyote ya mitishamba ambayo sijatumia kwa lengo la kupunguza uzito, hii huduma niliulizia nchi nyingine nikaona ina gharama kubwa,” alisema.

Hivi sasa Msechu alisema hali chakula kingi kama awali.
“Niliporudi nyumbani nilikuwa na kiu kali nikaambiwa maji niwe nakunywa kwenye kijiko, hivyo nilikunywa vijiko vinne, nilipoongeza cha tano nilitapika. Usiku nikanywa supu vijiko vitatu nilipoweka cha nne nikataka kutapika, hii ina maana kwamba tumbo linapokea chakula kidogo,” alisema Msechu.
Akizungumza kwa simu na Dk Muhumba mbele ya mwandishi, mgonjwa mwingine aliyepatiwa tiba hiyo alisema amepungua kilo 20 na ameondokana na maumivu ya mgongo yaliyokuwa yakimkabili.

“Maumivu ya mgongo yamepungua mno, sina changamoto hiyo kwa sasa, shida ninayokutana nayo ni tumbo kuvuruga na hii haitokei wakati wote, kuna muda najisikia vibaya ila kwa ujumla hali yangu ni nzuri ikilinganishwa na nilivyokuwa.

“Nilipima uzito mara ya mwisho juzi, nina kilo 130 kutoka kilo 150.8 nilizokuwa nazo.”


Wengine wanatamani

Mkazi wa Mbezi, Benjamin Ogweno alisema licha ya kusikia na kusoma mara kadhaa kuhusu njia hiyo ya kupungua hawezi kuiamini hadi atakapomshuhudia aliyeitumia na kufanikiwa.

“Wazungu wana mambo mengi na wanatuletea vitu vipya kila kukicha, nimeshawahi kusikia na kusoma mara kadhaa mtandaoni kuhusu hili puto. Kama kweli litakuwa na matokeo hayo basi sio mbaya hata gharama yake ingeshuka zaidi ili wengi tuweze kumudu, maana suala la uzito mkubwa ni kama janga la taifa,” alisema Ogweno.

Mkazi wa Chang’ombe, Sheila Jongo (32) alionyesha matamanio makubwa ya kupata tiba hiyo kukabiliana uzito alionao wa kilo 96.
“Nina asili ya unene tangu utotoni, lakini kadiri ninavyozidi kukua naona hali inazidi kuwa mbaya, nimejaribu haya mambo ya ‘diet’ kiukweli sijapata mafanikio. Hizi habari za puto zinaleta matumaini kwangu maana nimeshamuona mtu ambaye amefanikiwa kupitia njia hii. Kitakachonisumbua ni pesa ila kama nikipata nitaweka tu,” alisema Sheila.