Abiria Mwendokasi wafunguka, Dk Kihamia ahaidi kutatua kero

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Dk Athumani Kihamia (kushoto) akizungumza na abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa mabasi hayo alipokuwa kwenye ziara yake ya kwanza ya kutembelea miradi ya DART, jijini Dar es Salaam leo, Januari 25, 2024. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mtendaji mkuu mpya wa Dart, Dk Athumani Kihamia ameahidi kufanyia kazi malalamiko ya watumiaji wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka ili wafaidike na usafiri huo.

Dar es Salaam. Watumiaji wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) wamewasilisha baadhi ya kero kwa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, Dk Athuman Kihamia, ikiwemo kukaa muda mrefu vituoni kusubiri mabasi.

 Kero nyingine ni pamoja na abiria kujaa kupita kiasi kwenye mabasi hayo, safari kukatishwa njiani, wakisema kero hizo zinawachelewesha kufika kwenye majukumu yao ya kila siku.

Wakizungumza leo Januari 25,2024 wakati Dk Kihamia alipofanya ziara yake ya kwanza ya kikazi kuona mradi huo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Januari 11, 2024  akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Dk Edwin Mhede ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Wamesema changamoto hizo ni za muda mrefu na watendaji wa taasisi hiyo wanajua hasa kuanzia asubuhi wanapokwenda kazini na jioni wanaporudi nyumbani, lakini hawaoni maboresho.

“Mkono wangu wa huu wa kulia ulipata shida kwa sababu abiria ni wengi na tunajaa kupita kiasi, hivyo tunaomba kujua kwa kuwa ni mtendaji unatusaidiaje? Mimi nategemea usafiri huu kwenda Feri kuchukua samaki kila siku,” amesema Veronika Thobias, mkazi wa Mbezi

Amesema kuna wakati wanatoka Mbezi mabasi yanawashusha kituo cha Kimara, huku akieleza madereva wanawaeleza safari inaishia hapo.

“Tunaomba kujua inakuwaje abiria tuko wengi tumejaa kituoni, mabasi yamesimama karibu na ukiangalia ndani hakuna abiria, tunapitia shida tunaomba msaada wako,” amesema.

Naye Feisal Said amesema kukatishwa safari kuna wapotezea muda, huku akimuomba mtendaji huyo kuwafikiria kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Mbezi hadi Kivukoni kuwaepushia usumbufu.

“Kiongozi mtusaidie tunapata shida basi linaanzia Mbezi linakuja kushusha abiria hapa Kimara na tunakaa muda mrefu kusubiri lingine. Tunaomba mfikirie kuanzisha safari za moja kwa moja kupunguzia usumbufu na gharama,” amesema.

Kutokana an maswali hayo ya watumiaji, Dk Kihamia ameahidi changamoto zao kuzifanyia kazi moja baada ya nyingine, huku akipiga marufuku mtindo wa madereva wa mabasi hayo kuacha abiria vituo vyenye abiria wachache kwa kisingizio cha kuwahi vituo vyenye abiria wengi.

 Amesema ameshatoa somo kwa madereva hao, hivyo hategemei kuona abiria wakiachwa kwenye vituo wakisubiria usafiri.

“Tumepiga marufuku mtindo wa madereva kuacha abiria kwenye vituo vyenye abiria wachache kwa madai ya kukimbilia vituo vilivyopo na abiria wengi.

“Kwa mfano devera anaenda Fire anawapita watu Manzese, hiki kitu hakikubaliki hata kidogo na hakitajirudia tena,” amesema.

Dk Kihamia amesema licha ya kusikia malalamiko hayo kutoka kwa abiria, ameshamfikishia kero hizo Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa.

Amesema madereva hao wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali ikiwemo zamu zao zimeisha na kwamba wanakwenda kubadilishana na wenzao, huku akieleza ameshatoa somo na wameshamuelewa, hivyo changamoto hiyo haitajirudia.

“Walengwa wetu ni wananchi wanaotakiwa wanufaike na tumejipanga kila siku tutakuwa Mbezi na Kimara, ili kuona abiria wanajipanga kuingia kwenye mabasi na kuhakikisha yanaondoka haraka kuwaisha abiria,” amesema Dk Kihamia.

Dk Kihamia aliyekuwa ameambatana na watendaji wa taasisi hiyo amesema licha ya mradi huo kuwa na changamoto nyingi, lakini wamejipanga kuona zinatatuliwa mapema ili kurejesha huduma bora kwa watumiaji.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi malengo yetu ni kuona kero zilizopo zinatatuliwa kwa wakati,” amesema Dk Kihamia.

Kuhusu kuanzisha safari za moja kwa moja, Dk Kihamia amesema wana mpango wa kuanzisha safari hizo, akitoa mfano mabasi yaanzie Mbezi hadi Gerezani au Mbezi hadi Kivukoni, baada ya kuongezeka mabasi mengine mapya.

 “Nimepokea maombi ya abiria wengi wakitaka usafiri wa moja kwa moja na tumeona ni kweli mabasi yakishaongezeka tunafikiria kuanzisha safari hizo kuleta unafuu kwa wananchi na muda si mrefu tutawatangazia,” amesema.