Abiria wahaha kusaka usafiri kwenda Rombo
Muktasari:
- Adha ya usafiri imesababisha ongezeko la nauli kutoka Sh5, 000 hadi Sh7,000 kwenda maeneo ya Mkuu na Sh10,000 kwa wake wanaoenda Tarakea wilayani Rombo.
Moshi. Abiria wanaosafiri kutoka mjini Moshi kwenda maeneo ya Rombo, mkoani Kilimanjaro leo Jumapili Desemba 24, 2023 wamekumbana na adha ya kukosa usafiri kutokana na ongezeko la abiria wanaokwenda kusherehekea sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya.
Adha hiyo ya usafiri imesababisha ongezeko la nauli kutoka Sh5, 000 hadi Sh7, 000 kwa wanaoenda Mkuu na Sh10, 000 kwa Tarakea wilayani humo.
Mwananchi limeshuhudia ongezeko la abiria katika stendi ya Moshi kwa wale wanaoingia na kutoka, huku wengine wakizunguka kutafuta usafiri.
Beatus Mlanya ambaye ametokea Arusha na anasafiri kuelekea Rombo, amesema amefika kituoni hapo mapema mchana lakini hadi jioni bado hajapata usafiri, kwa kuwa magari aliyoyakuta yalikuwa tayari yamejaa abiria, huku nauli ikiongezeka mara mbili.
Mwenyekiti wa wenye magari yaendayo Rombo, Alfani Kupaza amesema licha ya uwepo wa magari zaidi ya 100 kutoka Moshi kwenda Rombo, kwa leo abiria wamekuwa wengi na kusababisha magari hayo kushindwa kukidhi mahitaji yaliyopo.
"Kwa siku ya leo abiria ni wengi sana, yapo magari zaidi ya 100 yaendayo Rombo, hivyo kunahitajika mengine ili kuondoa msongamano uliopo hapa stendi kwa sasa," amesema Kupaza.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Michael amesema wamejipanga kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo kwa kutoa vibali kwa magari binafsi na magari yaendayo njia nyingine ili yasafirishe abiria kwenda maeneo yenye changamoto ya usafiri.
Ali Said ambaye ni dereva wa magari yaendayo mkoani Arusha amesema tayari amepewa kibali cha kusafirisha abiria kwenda Rombo na kuwa ameonywa nauli isizidi Sh7, 000.