Undani msaada safari za usiku mabasi

Mwanza/Dar. Wakati zimesalia siku tatu kabla ya Krismasi na siku 10 kuhitimisha mwaka 2023 na kukaribisha mwaka mpya wa 2024, usafiri wa kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali, hali ni shwari tofauti na miaka mingine inavyokuwa.

Mwananchi ilifika Kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Magufuli kilichopo Mbezi, kwa siku mbili mfululizo na kuona hali ya usafiri ikiwa salama pasi na purukushani zilizozoeleka nyakati kama hizi.

Akizungumzia hali hiyo jana kituoni hapo, Ofisa Habari wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustapha Mwalongo alisema abiria wengi hivi sasa wanasafiri na mabasi ya usiku baada ya Serikali kuruhusu safari za saa 24.

Alisema ruhusa hiyo imetoa wigo mpana kwa abiria kuchagua muda wa kuanza safari na hivyo kwa sasa ni wachache wanaohitaji kusafiri kuanzia asubuhi.

“Ukifika hapa kituoni hawa abiria wote unaowaona wanaondoka na mabasi yanaanza safari kuanzia saa mbili na saa nne asubuhi na wapo wanaoondoka saa sita mchana na saa tisa alasiri,” alisema.

Akizungumzia hilo, Katibu wa Chama cha Umoja wa Madereva wa Mabasi, Abdallah Lubara alisema safari za saa 24 zimewapa Watanzania uhakika wa kusafiri wakati wowote kwa sehemu wanayotaka kwenda, tofauti na zamani walipolazimika kuondoka wakati mmoja na kuleta msongamano.

“Ili usafiri, ni lazima ukate tiketi siku moja kabla, lakini siku hizi watu wanakata tiketi mtandaoni na wanaondoka muda wanaotaka, kipindi kile kulikuwa na muda maalumu wa kuondoka, kulikuwa kunasababisha mrundikano wa abiria hapa standi,” alisema.

Alisema mrundikano huo ulikuwa chanzo cha watu kulanguliwa tiketi, jambo ambalo kwa sasa ni gumu kutokea.

Hata hivyo, wakati haya yakitokea katika stendi ya Magufuli, taarifa za matukio kadhaa ya ajali za barabarani ndani ya mwezi huu zimeripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi zikitajwa kutokana na safari hizo za usiku.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wa sekta ya usafirishaji wametaja sababu zinazochangia ajali hizo katika kipindi hiki cha safari nyingi za watu kwenda mapumziko kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, ikiwamo safari za usiku.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa ajali nyingi hivi sasa zinahusisha magari binafsi, tofauti na siku za mwanzo zilipokuwa zinahusisha zaidi mabasi ya abiria.
Inaelezwa jumla ya ajali 46 zilizosababisha vifo 46 na majeruhi 59, zimeripotiwa kutokea kati ya Desemba mosi hadi 12, mwaka huu.
 

Hakuna kulala kilio

Kutokana na usafiri huo, wamiliki wa mabasi madogo maarufu kama hakuna kulala wanaofanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali, ikiwemo Mbeya, Mwanza na Arusha wamelalamikia kukosa abiria kutokana na safari za saa 24.

“Miaka yote ikifikia kipindi kama hiki tulikuwa tunapata abiria wengi wanaohitaji kusafiri, lakini safari hii biashara imekuwa ngumu, hakuna abiria kabisa, wengi wanapanda mabasi ya kawaida,” alisema Sebastian Joseph.

Sebastian, miongoni mwa wamiliki wa mabasi ya Coaster alisema alikuwa na magari yaliyokuwa yanaenda mikoa mitatu Mbeya, Mwanza na Arusha, lakini kwa sasa amesimamisha shughuli hiyo kwa kukosa wateja.

Mmiliki mwingine, Salum Saedy alisema kabla ya kuanzishwa kwa safari za saa 24 walikuwa na sehemu maalumu za kupakia abiria kama Ubungo, Mbezi na Kibaha, lakini kwa sasa hakuna hata anayewapigia simu kuulizia, hivyo biashara imekuwa ngumu.

Kuhusu hilo, Mwalongo alisema walitegemea hali hiyo kujitokeza baada ya Serikali kuruhusu safari za saa 24.

“Tuliiomba Serikali kwa muda mrefu iruhusu kufanya safari za saa 24, kwa sababu ‘hakuna kulala’ zilikuwa zinasafirisha abiria wengi usiku na ikifika asubuhi kuna wakati tulikuwa tunapata abiria wachache,” alisema.

Katibu wa Chama cha Madereva wa Mabasi nchini (Uwamata), Abdallah Lubara alisema kwa sasa abiria wana wigo mpana wa kuchagua usafiri kwa kuwa umekuwa mwingi na bora.

“Hata wamiliki wa magari wameanza kushindana kuboresha huduma wanazotoa na ukiangalia kwa sasa abiria wengi wanafanya safari zao usiku,” alisema.

 

Sababu za ajali

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi alisema ajali nyingi hutokana na sababu za kibinadamu, uchakavu wa vyombo na uduni au kuharibika kwa miundombinu ya barabara.

“Ulevi wakati wa safari, uzembe, uchovu wa safari ndefu, kutojali au kutotii sheria ni baadhi tu ya sababu za kibinadamu zinazosababisha ajali,’’ alisema Ng’anzi.

Mwenyekiti wa Madereva wa mabasi na malori, Shubert Mbakizao alisema kukosekana kwa weledi na uzalendo miongoni mwa watendaji na viongozi wenye dhamana ya usimamizi na utekelezaji wa sheria kunachangia ajali za barabarani.

Alitaja sababu nyingine ni baadhi ya wamiliki wa mabasi kukiuka sheria kuhusu muda wa kazi, mishahara, posho na masilahi mengine kwa madereva.

“Kwa mfano, hivi sasa kuna mabasi yanayosafiri usiku yanatakiwa kuwa na madereva wawili, lakini mengi yana dereva mmoja au wa pili ni ‘tegesha’ tu, kwa sababu haendeshi gari mwanzo hadi mwisho wa safari,’’ alisema Mbakizao.

Alisema wengi wa madereva wa pili ni watu wasio na ujuzi wala uzoefu wa safari ndefu kwa sababu ni vijana wanatumika kusogeza na kugeuza magari kwenye vituo vya kuoshea magari na wanatumika kukwepa gharama ya mishahara na posho kwa madereva wawili.

Kuhusu uchovu, Mbakizao alishauri dereva wa pili akae kwenye kituo cha kupokezana ili kumwepusha na uchovu wa safari badala ya kuwa sehemu ya abiria ndani ya basi. Hata hivyo, mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania, Majura Kafumu alisema kukosa mikataba na mishahara kunawafanya madereva kuendesha wakiwa na msongo wa mawazo; na hivyo kusababisha ajali.

“Mishahara na posho za madereva ni midogo na wanalipwa mikononi badala ya benki; hawa ni lazima watakosa umakini barabarani kutokana na msongo wa mawazo,’’ alisema Majura.

Faini za makosa ya usalama barabarani kuwa sehemu ya mapato ya Serikali, askari kujificha vichakani kupiga picha za magari yanayozidisha mwendo, viongozi wa Serikali na wanasiasa kuwa wamiliki mabasi na askari polisi kujadiliana na kuelewana na madereva wanaokiuka sheria ni sababu nyingine inayotajwa kuchangia ajali.

“Wapo madereva wanaoweka tayari fedha kwa ajili ya ama kumalizana na askari wa usalama barabarani au kulipa faini,’’ alisema Majura.
 

Nini kifanyike kudhibiti ajali

“Ajali zote zinaweza kuzuilika iwapo kila mtu kuanzia madereva, wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, mamlaka za usimamizi wa sheria, abiria na wadau wengine wote watatimiza wajibu,’’ alisema Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi.

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria na ukaguzi wa mara kwa mara na matumizi ya mifumo na teknolojia kudhibiti ajali na kuwa hili si kwa kipindi hiki pekee, bali ni kazi endelevu.

“Malengo ya Jeshi la Polisi ni kuona mtumiaji wa barabara popote na wakati wote wanatii sheria,’’ alisema Ng’anzi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo alisema tayari matumizi ya kitufe cha utambuzi na mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS), imeanza kutumika kusaidia si tu kuongeza umakini kwa madereva, bali pia kupunguza ajali.
 

Treni kaskazini yafurika

Wakati abiria wa usafiri wa mabasi wakipata ahueni, changamoto ya usafiri kwa sasa imehamia kwenye usafiri wa treni inayoenda Kaskazini, ambako imeonekana wasafiri kuwa wengi.

Kiwango cha nauli kinachotozwa ni moja ya sababu za ongezeko la wasafiri wanaokimbilia njia hiyo kwa sasa, baada ya kauli za mabasi kupanda.
Sh31,000 anazolipa abiria wa basi kwa daraja la kawaida kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, akisafiri na treni analipa Sh19,000 kwa daraja la tatu na hivyo anakuwa ameokoa Sh12,000.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk alisema kutokana na ongezeko la mahitaji, ratiba ya usafiri huo imebadilika wiki hii na safari zinafanyika mara tatu kwa wiki, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

“Ninavyoongea kuna treni inaondoka saa tisa alasiri, idadi ya abiria ni wengi na kwa siku za kawaida tunatumia mabehewa sita, lakini kwa siku ya leo (jana) tumeongeza kuna manane na abiria wengi wamebaki,” alisema.

Jamila alisema kwa safari ya kesho Ijumaa wanatarajia kuongeza mabehewa kufikia 16 ya abiria na wakizidi kiwango hicho wataongeza treni maalumu kwa ajili ya kuwapeleka.

Alisema kila ifikapo Desemba kila mwaka mahitaji ya abiria wanaohitaji usafiri huo huwa ni wengi lakini safari hii mwanzoni walisimama kidogo kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea.