Serikali imalize utata wa nauli mpya mapema

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza ongezeko la nauli kuanzia Desemba 8, baada ya kutokuwepo pingamizi lolote kutoka kwa wadau wa usafirishaji.

Ongezeko hilo la nauli linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya vipuri, mafuta pamoja na changamoto ya upatikanaji wa sarafu ya Dola ya Marekani.

Kwa kawaida mabadiliko ya viwango vya nauli hufanyika baada ya mamlaka husika kupokea maombi kutoka kwa watoa huduma (wamiliki) wakihitaji viwango vya nauli vifanyiwe marejeo.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra Habib Suluo alifafanua kuwa daladala zenye ruti isiyozidi kilomita 10 nauli itapanda kutoka Sh500 hadi Sh600, ruti ya kilomita 11 hadi 15 nauli itaongezeka kutoka Sh550 hadi Sh700 na ruti ya kilomita 16 hadi 20 nauli itaongezeka kutoka Sh600 hadi Sh800.

Alisema daladala zilizokuwa na ruti ya umbali wa kilomita 21 hadi 25 nauli itapanda kutoka Sh700 hadi Sh900, na zile zenye ruti ya kilomita 26 hadi 30 nauli itapanda kutoka Sh850 hadi Sh1,100.

Taarifa hiyo pia ilieleza, kuwa daladala ambazo zilikuwa zinatoza Sh1,000 (umbali wa kilomita 31 hadi 35) bei itapanda hadi Sh1,300 na zile zenye ruti ambazo umbali wake ni kati ya kilomita 36 hadi 40, bei ya nauli itapanda kutoka Sh1,100 hadi Sh1,400.

Hata hivyo wakati nauli za daladala zikipanda kwa wastani wa asilimia 10, pia nauli za mabasi ya masafa marefu zimepanda kulingana na daraja la basi na aina ya barabara zinayotumika.

Mfano mabasi ya daraja la kawaida katika barabara za lami kila kilomita moja itatozwa Sh48.47 kutoka Sh41.29 kama ilivyokuwa awali na kwa barabara ya vumbi daraja hilo litatoza nauli ya Sh53.32 kwa kilomita kutoka Sh51.61.

Pia, nauli itapanda kwa mabasi ya daraja la kati (luxury na semi-luxury) kwa barabara ya lami nauli itapanda kutoka Sh56.88 kwa kilomita hadi Sh67.84.

Baada ya kuanza kutumika kwa viwango hivyo vipya, Meneja Leseni kutoka Latra, Leo Ngowi aliagiza daladala zote kubadilisha na kuandika nauli mpya kwenye milango ya magari, hata hivyo agizo hilo bado halijatekelezwa hali inayowafanya abiria kutojua kiwango hali cha nauli kilichoongezeka.

Kutotekelezwa kwa agizo hilo kumesababisha kuibuka mivutano kwenye vyombo hivyo vya usafiri, kutokana na baadhi ya makondakta kutoza viwango vya nauli, tofauti na bei elekezi iliyotangazwa na Latra.

Sio kwenye daladala tu, mvutano huu pia umeonekana kwenye mabasi yanayofanya safari za mikoani kutokana na kutobadilisha viwango hivyo kwenye mfumo wa tiketi mtandao (E- tiketi) na kusababisha abiria kutozwa viwango tofauti na bei elekezi.

Hapa kinachoonekana watoa huduma wamekuwa wakijificha kwenye kichaka cha matumizi ya tiketi za kawaida (vitabu) ambavyo mtu anaweza kuandika kiwango anachokitaka licha ya mamlaka kupiga marufuku hivi karibuni.

Kwa ujumla tangu bei mpya itangazwe abiria wengi, wamekuwa hawana uelewa wa mabadiliko hayo .

Mvutano uliopo sasa kati ya abiria na wasimamizi wa vyombo hivyo ni kutokuwa na orodha ya bei elekezi ndani ya gari kama sheria inavyoelekeza.

Sheria za Latra zinamtaka kila mtoa huduma kuhakikisha anakuwa au kubandika orodha ya viwango vya nauli, ndani ya gari, na kwa daladala inaelekeza kila ubavuni kwenye mlango kuandikwe kiwango sahihi cha nauli na sehemu husika linapoelekea.

Siwezi kuwatupia lawama, wamiliki wa vyombo vya moto hapa shida naiona ni kwa baadhi ya wahudumu wa vyombo hivi nikimaanisha makondakta na madereva kutumia fursa hii ya mabadiliko ya nauli kujinufaisha.

Hawa wamekuwa wakivutana na abiria mara kwa mara sababu zikiwa ni kuongeza nauli sehemu ambayo abiria alipaswa kulipa Sh700 au Sh800 wao watamzoza Sh1,000 jambo ambalo abiria hawakubaliani nalo.

Kinachotakiwa hapa kwanza mamlaka husika nikimaanisha Latra watoe elimu ya kutosha kwa abiria kuhusiana na mabadiliko ya nauli kwa kuwafafanulia umbali na bei.
Pili Mamlaka husika kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wafanye msako kubaini wale wote wanaokiuka sheria na taratibu ili kuepuka mvutano usiokuwa na tija.

Na mwisho watoa huduma wanapaswa kuzingatia sheria na tarabu zilizowekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuzingatia viwango halali vya nauli vilivyoidhinishwa na Serikali.
Mwandishi anapatikana kwa namba 0716287513