Abiria wakaa chini ili daladala kutokamatwa kukiuka agizo maambukizi ya corona

Muktasari:

  • Agizo la daladala kupakia abiria kulingana na idadi ya viti ili kupunguza wanaosimama kwa ajili ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona huenda halijaeleweka kutokana na baadhi yao kukaa chini kwenye mabasi hayo.

Dar es Salaam.  Agizo la daladala kupakia abiria kulingana na idadi ya viti ili kupunguza wanaosimama kwa ajili ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona huenda halijaeleweka kutokana na baadhi yao kukaa chini kwenye mabasi hayo.

Lengo la kukaa chini ni ili wao waweze kupata usafiri kuwahi katika shughuli zao na pia daladala husika kutokamatwa na askari wa usalama barabarani kwa kusimamisha abiria.

Katika daladala moja linalofanya safari zake kati ya Mbagala na Tabata Chang’ombe leo Jumanne Machi 31, 2020 Mwananchi imeshuhudia abiria zaidi ya 10 wakiwa wamekaa chini.

Baada ya abiria wote kuketi kwenye viti, kondakta aliwaita watu wengine na kuwasisitiza wakae chini ili wawahi kwenye shughuli zao.

Kutokana na adha kubwa ya usafiri abiria nao hawakuwa na hiana walijikunja na kukaa chini bila kujali usalama wao.

Kila kituo abiria walikuwa wakipanda na kushuka, wale waliopanda walitii agizo la kuketi chini.

Utaratibu wa abiria kukaa katika siti na daladala kutosimamisha abiria umekuja baada ya Mamlaka ya Udhibiti  wa Usafiri Ardhini (Latra) kuwataka watumiaji wa usafiri huo kutojazana kwa ajili ya afya zao.

Latra ilitoa agizo hilo Machi 19, 2020 ikiwa ni jitihada za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona ambavyo huweza kutokea kirahisi katika mikusanyiko ya watu, hasa katika usafiri wa umma.

Virusi hivyo husambaa kwa mtu mwenye maambukizi kukohoa au kupiga chafya na matone ya maji kumuangukia asiye nayo, au kuangukia sehemu  halafu mwingine kugusa eneo hilo na baadaye kutumia mikono kugusa usoni, ambako virusi hivyo hupenya mwilini kupitia mdomo, pua au macho.

Hivyo, wasafiri hutakiwa kuwa ndani ya basi lenye abiria wachache ili kuwa na nafasi baina ya abiria mmoja na mwingine.