Acheni Jide awe mwanamke na nusu

Kati ya tabia kerefu kwa totoz za Kibongo ni kutoheshimu miadi. Hawana utamaduni huo. Unapanga mkutane sehemu saa tisa alasiri. Anakuja saa kumi na moja jioni. Kibaya zaidi hana muda wa kuomba radhi, atafika na kuagiza savanna zake.

Uwapo baa muhudumu wa kike kila dakika atakusikiliza, ukiwa na demu unaanza kazi ya kumuita umuagize, demu naye akihudumiwa na demu mapozi mengi, atajivuuta utadhani hajui anachokunywa, huku mikono yake akirusharusha kuweka sawa kijora chake mabegani.

Siongelei wadangaji wa mjini. Hapana, anaweza kuwa mkeo au mpenzi, mnapanga kwenda sehemu saa tatu asubuhi lakini mpaka muda unafika yeye anajivutavuta. Mpaka mnakuja kuondoka saa nne. Hivi kwa nini wanawake wa Kibongo hamjali muda wa miadi?

Ili uende nao sawa acha mwanamke aseme yupo tayari ndo muondoke au kumuita sehemu. Unaweza kwenda naye Kariakoo mkazunguka maduka yote anachagua kila nguo na kila anachokiona halafu utasikia hii sijaipenda. Yaani kupotezeana muda tu.

Ukute kaanza kuoga yeye, baadaye anafuata mwanaume ajabu mwanaume anamaliza kujiandaa yeye bado. Ana nguo nyingi zaidi ya mume lakini haoni ya kuvaa. Totoz ipe saa mbili za kujiandaa, kama unataka mtoke saa 10 jioni, mwambie saa 8 mchana awe tayari.

Tuelezane ukweli. Kama ulikuwa hujui huu ndo ukweli wenyewe. Kuwa mademu wenye pesa au watoto wa kishua wana mapenzi ya dhati sana kuliko wasio nazo.

Huu ndo ukweli ambao nimeamua kuwachana ukweli. Kama hutaki shauri yako.

Toka nizaliwe hadi sasa nishakutana na totoz kadhaa. Na kati yao kuna masikini au watoto wa choka mbaya wa kutosha na wanaotokea familia za kitajiri. Yaani watoto wa kishua wa kutosha. Nafahamu tofauti ya choka mbaya na wa kishua.

Choka mbaya anakuja gheto hesabu zake zinalenga pochi yako. Yaani anaanza kukueleza shida zake utadhani wewe ndo ulimzaa.

Choka mbaya kwanza lazima akuache choka mbaya kimwili. Wanajituma mno kwenye sita kwa sita kama takrima. Pili anakuacha choka mbaya mifukoni kwa sababu wanataka usiku mmoja utatue matatizo yao yote. Mpaka ya wajomba zake wa huko Naliendelea.

Mtoto wa kishua anakuacha uko poa kimwili kwa sababu anafanya kwa starehe na siyo ajira. Pili anakuacha mifuko yako iko salama kwa sababu hawezi kukugeuza TATU MZUKA au BIKO yake. Yaani anakuacha salama mfukoni na anaweza kukulinda na chochote vile vile.

Tatizo lingine la totozi ni kupenda kusifiwa sana. Wanaume tunajua udhaifu mkubwa wa mademu ni sifa. Wanapenda kusifiwa na sifa nyingi ni za kijinga tu. Sasa wanaume hutumia njia hii kuwanasa, hata mke wa mtu mwenye wajukuu atapewa sifa nyingi na kujiona kigoli.

Ajabu ni kwamba huwa hawashangazwi na sifa za uongo wanazopewa mpaka kujiona malkia, wao huumizwa zaidi wasiposifiwa hata kama hawastahili hizo sifa. Muda wa kuwaza kuwa kuna wengine pia wanasifiwa hivyo hivyo, hawana.

Wanaume wengi hutumia hii ‘tekniki’ kuwapata wanawake kirahisi, na wanawake wengi huingia kichwa kichwa.

Mwanaume anaoa demu yeyote awe mzuri awe mbaya, anasifia demu yeyote awe mbaya au mzuri mradi apate utamu anaotaka. Sifa anazopewa mke ndizo anazopewa ‘hausi geli’ pale ibilisi anapochukua jukumu la kutawala kwenye akili za mwanaume.

Umesikia sakata la video na picha za utupu kwa baadhi ya wasichana wa mjini? Hiyo yote ni kutokana na sifa za kijinga. Msichana anasifiwa kwa sifa za uongo mpaka anaamua kuweka utupu wake hadharani. Ndo maana wanaume hawapatwi sana na majanga haya.

Dunia ya sasa inakupa kila kitu. Huhitaji kutumia nguvu kubwa sana ili kupata umaarufu. Mahitaji yote yanayoweza kukufanya uwe maarufu yapo. Mzungu kakusogezea fursa zote kupitia tekinolojia. Inashangaza kutafuta jina kwa njia haramu.

Miaka ya nyuma ili dunia ikutambue ilitakiwa ufanye zaidi ya uwezo wa kawaida wa binadamu. Adolf Hitler alikuwa maarufu zaidi kwa sababu wapo watawala walioua sana watu lakini yeye akapitiliza kiwango cha kawaida cha mauaji.

Mwanaume wa Kitanzania huko Uingereza kaua mwanamke mmoja, dunia imejua. Kafungwa maisha. Urahisi wa kujua tukio dogo lililofanyika maili nyingi kutoka ulipo, unaenda sawa na urahisi wa kudhibiti tukio kubwa. Watu sampuli ya Hitler hawatajirudia siku za usoni.

Dunia ipo kiganjani huwezi kufanya tukio bila kujulikana. Inashangaza totoz za mjini kujidhalilisha. Wakati kuna njia zaidi ya milioni za kuwapa umaarufu. Dunia ya sasa huhitaji kutumia nguvu nyingi sana kujulikana.

Wasichana wamekuwa wahanga wakubwa wa haya matukio. Kama ambavyo ni wazito kwenye miadi. Ndivyo wengi wao walivyo wazito kwenye maamuzi.

Wengi kupenda kwao sifa za kijinga ndio maana wanatumika kijinga. Wanapigwa picha za utupu kwa kusifiwa tu.

Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ alitumia nguvu nyingi sana ili ajulikane. Atambulike na muziki wake kupendwa kisha kumiliki ‘fan base’ kubwa Afrika. Haikuwa kazi ndogo. Na alichofanya siyo kiki za picha wala video za utupu mitandaoni.

Jide hakuwa muumini wa kuandikwa kwa skendo magazetini. Hakuwahi kuwa rafiki na kurasa za stori za udaku. Aliamini kwenye muziki wake. Akajikita kwenye muziki kwa kuwa aliamini hakuwa na njia nyingine ya kupaa kimafanikio zaidi ya muziki wake.

Wakati ule fursa za kujulikana zilikuwa finyu lakini alipasua. Bila kutegemea chochote zaidi ya mashairi na sauti yake. Hata jukwaani siyo mnenguaji. Sauti yenye mvuto na mashairi yenye ushawishi yakampa mafanikio. Jide ndo yule pale anasukuma ndinga anayotaka.

Jide alitoka dunia ya tatu huku ikiwa bado gizani. Ulimwengu huu ungewahi kufika nyakati zile dunia ingemkoma. Lakini hawa waliomfuatia baada yake walisombwa na mafuriko ya maendeleo. Wa kiume na wa kike wengi wako chali kifo cha mende. Jide yupo.

Mtoto aliyezaliwa wakati Jide anatoka kimuziki hivi sasa ameanza chuo kikuu. Jide yuko palepale hajawahi kushuka pamoja na misukosuko mingi ya maisha binafsi na biashara ya muziki. Kuwa Jide ni zaidi uwezo wa kawaida.

Amepita njia tofauti na wasichana wengi wasiojielewa. Jide kama angeshindwa kuzingatia muda kama tabia za wasichana wengi, huenda hii leo asingekuwa pale. Aliutumia muda vyema wa kuandika mashairi, kufanya mazoezi na kukesha studio.

Hakuwa mtoto wa kishua. Pia akawa tofauti na wasichana wa uswazi kutegemea pesa za wanaume. Akawa na hasira na maisha huku akiamini vita ya maisha angeshinda kupitia muziki. Akaweka nia na kuzingatia kazi yake hivi sasa anakula matunda.

Jide hakupenda sifa za kijinga. Wakati wasichana wa mjini wakipambana kupata nafasi za kuuza sura kwenye kurasa za udaku. Jide alijenga uadui na habari za udaku. Kasikilize nyimbo zake utaelewa. Angekuwa mpenda sifa angechafua sana kurasa.

Bado muda mfupi Jide afikishe miaka 20 kama staa wa kike namba moja Afrika Mashariki kwenye muziki. Wasichana wakitumia nguvu kubwa kutafuta jina katika dunia isiyohitaji nguvu kubwa kujulikana. Jide kaendelea kuwa yuleyule hajasombwa na ujinga wa sasa.

Kama hukwenda katika shoo yake aliyofanya karibuni. Hujaona mitandaoni wala runingani. Tafuta watu wakusimulie. Bonge la shoo na nyomi la kufa mtu bila kutegemea kiki za instagram. Ilikuwa sawa kuimba peku kwa furaha. Jide ni mwanamke na nusu.