ACT Wazalendo: Bunge lifanyie kazi maoni ya wadau

Muktasari:

  • Wakati mjadala kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi ukiendelea bungeni, ACT Wazalendo kimeutaka mhimili huo kutunga sheria kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wadau mbele ya Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Bunge kufanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau, ili kuboresha miswada ya sheria za uchaguzi inayoendelea kujadiliwa bungeni baada mchakato wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kusikiliza maoni ya wadau.

Chama hicho kimetoa wito huo kwa Bunge ikiwa imepita siku moja tangu kamati hiyo ilipowasilisha taarifa yake bungeni baada ya kukusanya maoni ya wadau kuhusu namna ya kuboresha miswada hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari mosi, 2024, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema kamati imechukua baadhi ya maoni ya wadau, lakini imeyaacha mengine ya muhimu, hivyo kazi imebaki mikononi mwa Bunge kuhakikisha mambo muhimu yanaingizwa kwenye sheria husika.

“Bunge linapaswa kufanyia kazi maoni ya wadau na kuhakikisha yale masuala ambayo hayajapata mwafaka wa kitaifa na yanakubalika na wadau wengi yanajumuishwa kwenye miswada yote mitatu.

“Nimesikiliza kwa makini uchambuzi wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria juu ya maoni ya wadau, tumeona baadhi ya maeneo machache yamechukuliwa ikiwemo yale ambayo ACT Wazalendo tuliyatolea maoni na kwa msisitizo ni lile la wakurugenzi wa halmashauri kutokuwa wasimamizi wa uchaguzi,” amesema Shaibu.

Amesema kamati pia imechukua maoni ya kupanua wigo wa wapigakura hususani kwa wafungwa kuruhusiwa kupiga kura. Amesema ingawa kamati haikuhitimisha suala la diaspora kupiga kura, lakini ni hatua nzuri.

Hata hivyo, amesema yapo maoni mengi ya wadau vikiwemo vyama vya siasa, hayajachukuliwa katika ngazi ya kamati, amelitaka Bunge kuhakikisha maoni yote yaliyoleta umoja wa kitaifa, yaingizwe kwenye sheria.

“Tunafuatilia mjadala unaoendelea bungeni katika miswada hii mitatu, bado masuala haya hayajapewa uzito wa kipekee. Mfano mmoja wapo ni usimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa unapaswa kutoka Tamisemi kwenda Tume ya Uchaguzi,” amesema Shaibu.

Amesema vifungu vyote vya sheria ya vyama vya siasa vinavyoijinaisha siasa viondolewe na pia mfumo wa ugawaji ruzuku unapaswa ubadilishwe, kuwe na mifumo miwili; kwanza, ruzuku kutolewa kulingana na matokeo ya uchaguzi; pili, asilimia fulani ya ruzuku igawanywe kwa vyama vyote vya siasa ili kuviimarisha.

“Mfano mwingine ni hiyo kamati ya usaili ya Tume, ni lazima kuhakikisha ushiriki wa asasi za kiraia na vyama vya siasa kwenye kamati ya usaili kwa sababu ilivyo sasa watu wengi waliomo mle ni wateule wa Rais.

“Kwa ujumla, Bunge lifanye wajibu wake wa kumalizia uingizwaji wa maoni ya wadau kwenye miswada hiyo,” amesema katibu mkuu huyo wa ACT Wazalendo.

Wakati ACT Wazalendo kikitoa wito huo, vyama vingine vya siasa vimeipongeza kamati kwa kuchukua maoni muhimu ya wadau, jambo ambalo wamesema linawapa imani kwamba watapata sheria nzuri.

Mwenyekiti wa Ada-Tadea, Juma Ali Khatibu ameipongeza kamati ya Bunge kwa kuzingatia baadhi ya maoni ya wadau hasa vyama vya siasa na asasi za kiraia, kwani yapo mambo yamechukuliwa na kufanyiwa kazi.

Amesema suala la wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi ni moja ya mambo yaliyochukuliwa pamoja na upatikanaji wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na makamu wake pia limezingatia.

“Tunaipongeza kamati ya Bunge kwa kuchukua baadhi ya mambo, ingawa kuna mambo mengine hayajachukuliwa. Mfano suala la ruzuku kwa vyama vya siasa, lakini hatujavunjika moyo, yapo yaliyochukuliwa, yapo ambayo hayakuchukuliwa.

“Huwezi kupata yote mia kwa mia, lazima mengine yatakwenda, mengine yatabaki. Kwa hiyo, haya tuliyopata, niseme tu nalipongeza Bunge letu na Serikali yetu kwa kuwa sikivu, ni imani yetu kuwa tutafika na hayo yaliyobaki yatafanyiwa kazi,” amesema Khatibu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo amesema kamati imezingatia maoni ya wadau kwa kiwango kikubwa ikiwemo suala la wakurugenzi kutosimamia uchaguzi, jambo lililokuwa likilalamikiwa na wadau kwa muda mrefu.

Amesema suala la mabadiliko ya jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wadau wengi walipendekeza iitwe Tume Huru ya Uchaguzi, ameona kamati kwenye taarifa yake wamelichukua hilo, kwani halivunji katiba ya nchi na halina ukakasi wowote.

“Kulikuwa na vifungu vinavyomtaka mpigakura anapotaka kuhuisha taarifa zake kwenye daftari la wapigakura aweze kulipia, lakini mapendekezo ya muswada ni kwamba suala hilo lisiwepo na Serikali wakati inawasilisha imekubaliana na hoja ya kamati.

“Kwa hiyo nimeona kwa kiasi kikubwa maoni ambayo yametolewa yamezingatiwa kwa asilimia kubwa,” amesema Doyo alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusu uzingatiwaji wa maoni ya wadau kwenye miswada mitatu iliyowasilishwa bungeni.