Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo kutinga mahakamani kupinga Sheria ya Fedha 2026

Naibu Waziri Mkuu katika Baraza Kivuli la ACT- Wazalendo, Luhaga Mpina

Muktasari:

  • Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge takribani wiki moja iliyopita huku likifanya marekebisho kadhaa katika maeneo yaliyopendekezwa na Kamati ya Bajeti pamoja na baadhi ya wabunge akiwano mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeanza mchakato wa kufungua shauri mahakamani kupinga vifungu vya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2026 kwa madai kwamba, vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuongeza mzigo kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 30, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Mkuu katika Baraza Kivuli la ACT- Wazalendo, Luhaga Mpina wakati akitoa msimamo wa chama hicho baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, bungeni Dodoma.

Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge takribani wiki moja iliyopita huku likifanya marekebisho kadhaa katika maeneo yaliyopendekezwa na Kamati ya Bajeti pamoja na baadhi ya wabunge akiwano Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT), Ado Shaibu.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyokubaliwa ni kuondolewa kwa ongezeko la tozo kwa pikipiki, ushuru wa kilo ya sukari inayozalishwa ndani ya nchi na marekebisho ya kodi zilizokuwa zikihusu magari yaliyotumika, hatua zinazotarajiwa kutoa nafuu kwa wananchi na sekta husika.

Mpina amesema ACT- Wazalendo imebaini ukiukwaji huo wa sheria unaohusu kuanzishwa kwa kodi zisizo na tija, utoaji wa misamaha ya kodi usiozingatia uwazi na masilahi ya Taifa, matumizi mabaya katika sekta ya mafuta yaliyosababisha hasara kwa uchumi, pamoja na uchukuaji wa fedha za mifuko maalumu kinyume cha Katiba na sheria.

“Tutafungua mashauri mahakamani kupinga vifungu vya Sheria ya Fedha, 2026 vinavyokiuka Katiba, kupinga misamaha ya kodi isiyo halali, kupinga marekebisho yanayohalalisha uchukuaji wa fedha za mifuko maalumu, na kudai kurejeshwa kwa fedha zote zilizochukuliwa au kutumika kinyume cha sheria," amesema mwanasiasa huyo aliyejiunga na chama hicho akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ametoa wito kwa wananchi, taasisi za kikatiba na wapigania haki katika kulinda Katiba, utawala wa sheria na rasilimali za Taifa.

 Amesema ACT- Wazalendo itaendelea kutumia njia zote halali za kikatiba na kisheria kuhakikisha fedha za wananchi zinalindwa, sheria zinaheshimiwa na Serikali inawajibika kwa kila uamuzi unaogusa maisha ya Watanzania.

“Msimamo wa Chama cha ACT -Wazalendo ni kwamba, vifungu vya 10, 22, 83 na 94 vya muswada vifutwe ili kuliwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake na kuondoa utoaji holela wa misamaha ya kodi unaopoteza mapato mengi ya Serikali.”


Wasiyokubaliana nayo

Mpina amesema ACT haikubaliani na kitendo cha Serikali kuja na tozo ya asilimia 10 kwa nyavu zinazozalishwa nje ya nchi kwani katika mapendekezo yake kiliitaka Serikali iondoe tozo hiyo, lakini hakuna maboresho.

“Serikali imependekeza kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye matairi mapya ya pikipiki, tukapendekeza ushuru huu ufutwe ila hakuna maboresho. Ada hii haina tija na inaongeza gharama kwa wananchi wanyonge hasa bodaboda hivyo, kuua ajira na uchumi, ACT hatukubaliani,” amesema.

Mpina amesema ACT haikubaliani na Serikali kuongeza tozo ya uchakataji wa nyaraka za kuingiza bidhaa nchini kutoka asilimia 0.6 hadi 1.

Amesema ongezeko la tozo lifutwe na hakuna maboresho ijapokuwa tozo hiyo haina tija na inaongeza gharama kwa mlaji wa mwisho.

Hata hivyo, amesema chama hicho kinakubaliana na pendekezo la Serikali kuanzisha ushuru wa bidhaa wa asilimia tano kwa pikipiki zinazotumia mafuta huku pendekezo lao likitaka Serikali iondoe ushuru huo huku matokeo yake yakifutwa na Serikali.

“Katika muswada, Serikali ilianzisha tozo ya Sh10 kwa kila kilogramu ya sukari ya ndani na ya nje kwa ajili ya kugharamia Mfuko wa Bima ya Afya. Tulitoa maoni Serikali iondoe na Serikali imefanya marekebisho kwa kuondoa tozo hiyo, badala yake imeweka tozo ya Sh20 kwa sukari inayoingizwa nchini, tunakubaliana,” amesema.


Wanayokubaliana nayo

Miongoni mwa mambo yaliyofanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo ambayo ACT - Wazalendo kinakubaliana nayo ni Serikali kuondoa Kifungu cha 11(g) ya Sheria ya Fedha, wakiitaka Serikali iondoe ushuru wa bidhaa wa asilimia 5 wa pikipiki, jambo ambalo limefanyika.

Serikali ilipendekeza kuanzisha ushuru huo, lakini ilikubali kuondoa pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye pikipiki kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye Kifungu cha 11(g) cha Muswada.

Vilevile, ACT Wazalendo kinakubaliana na uamuzi wa Serikali kufanya marekebisho kwa kuondoa tozo ya Sh10 kwa sukari inayozalishwa nchini iliyopendekezwa kjwenye muswada. Awali, chama hicho kilipendekeza kuondolewa kwa tozo hiyo, jambo ambalo limefanyika.

Chama hicho kinakubaliana na pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia moja (1) kwenye malipo yanayohusu mazao ya kilimo, wanyama hai, maziwa, Samaki, na mabondo kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye Ibara ya 25 ya Muswada.

“Serikaliki imefanya marekebisho kwa kufuta Ibara ya 5 yenye mapendekezo ya kurekebisha kifungu cha 69. Tunakubaliana.”