ACT Wazalendo walia na gharama za maisha

Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amesema bado hali ya maisha ngumu na hakuna dalili ya ahueni kwa wananchi hasa wanaoishia vijijini.

Kilwa. Chama cha ACT- Wazalendo, kimeendelea kukomalia suala gharama za maisha hasa upandaji wa bei za vyakula, kikisema hali hiyo ikiendelea itawaathiri wananchi hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa jana Mchi 10 na Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika uwanja wa Maalim Seif Sharif Hamad Garden Kilwa Kivinje mkoani Lindi.

Semu aliyeongozana na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwemo Zitto Kabwe na Juma Duni Haji, amesema bado hali ya maisha ngumu na hakuna dalili ya ahueni kwa wananchi hasa wanaoishia vijijini.

"Tunaelekea kwenye mfungo wa Ramadhani hali bado ngumu kwa wananchi wetu, hatujuhi kama familia zitaweza kumudu gharama kupata futarii, sijui itakuaje.

"Kila tunapopata nafasi ACT - Wazalendo tunaieleza Serikali kuhusu ugumu wa maisha lakini inatoa sababu za vita kati ya Ukraine na Urusi au suala la Uviko- 19.Jamani Taifa lolote wananchi wake wasiojiweza linakuwa katika hali ngumu," amesema Semu.

Mwezi uliopita Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe walisema changamoto ya mfumuko wa bei za vyakula itadumu kwa muda mchache kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali

"Haya (mazao) tunayotumia sasa hivi ni yale yaliyozalishwa mwaka jana, yaliyozalishwa kwa mbolea isiyokuwa na ruzuku, maana yake walitumia Sh120,000 hadi Sh140,000, mafuta hayakuwa na ruzuku, ndiyo yaliyokuwa juu na yalitumika katika usafirishaji na uzalishaji katika baadhi ya maeneo,” alisema Dk Mwigulu.

Lakini katika mkutano huo, Semu amedai kuwa kutokana na ugumu wa maisha ili mwananchi anunue mchele basi inamlazimu kuuza korosho kilo tatu ili kununua bidhaa hiyo.Alisema watu waliokuwa wanakula milo miwili hivi sasa wanakula mlo mmoja.

"Serikali inapaswa kuachia chakula kutoka kwenye maghala na ihakikishe kinawafikia wananchi hasa wa maeneo ya vijijini, ingawa imeachia mahindi lakini sio wananchi wote wamenufaika na ahueni hiyo.

"Pia Serikali ihakikishe zile tani 90,000 za mchele zitakazoagizwa kutoka nje inazisimamia vema kwa kuhakisha wananchi wanapata kwa wakati chakula hicho," amesema Semu.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji maarufu Babu Duni alisema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mambo yamebadilika, akisema miaka saba iliyopita ilikuwa ngumu mikutano ya hadhara kufanyika kwa ajili ya kusikiliza kero kwa wananchi.

"Wananchi wa Kilwa na Lindi endeleeni kusimama na ACT katika kudai mabadiliko ambayo Rais Samia ameanza kuyaonesha lakina inapaswa kuhimizwa ili kufikia mabadiliko hayo ikiwemo sheria mpya za uchaguzi," amesema Duni.

Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara 'Bwege' mesema ziara ya viongozi wakuu wa chama hicho, inalenga kuwakumbusha wananchi wa Lindi kwamba wasikate tamaa, akisema mapambano ya kisiasa bado yanaendelea.

"Tumekuja kuwambusha na sio kuwazindua, maana nyie mlishazinduka mapema ila tunakumbusha msikakate licha ya madhila yaliyotokeza ndani ya miaka saba iliyopita," amesema Bwege aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kuanzia mwaka 2010 hadi 2020.

Katika mkutano huo, Bwege ambaye alikuwa kiongozi wa wabunge wa mikoa ya kusini kwa nyakati tofauti, alisema atatoa gari lake aina Canter litumike kwa ajili ya shughuli za chama katika wilaya ya Kilwa.Alisema wakati huu ni wakati wa mapambano ya kuimarisha chama hicho.

"Leo nina ahueni lazima nikisaidie ACT- Wazalendo, sina uwezo wa kumpa mtu fedha, bali natoa zawadi ya gari kwa Kiongozi wa Chama (Zitto) kwa ajili ya kuimarisha shughuli za chama ili kutetea maslahi ya wana Kilwa ikiwemo changamoto zinazowakabili," amesema Bwege.

Kwa upande wake, Zitto amemshukuru Bwege kwa zawadi hiyo na kumuahidi kuwa watafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuimarisha chama hicho na ikifika msimu wa uchaguzi wachukue vitongoji mitaa na majimbo yote mawili ya wilaya hiyo.