Adaiwa kujiteka ili apate fedha ya kulipa deni

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia  mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa kutoa taarifa za ndugu yake aitwaye Dickson Peter Mungulu kutekwa baada ya kupokea ujumbe mfupi simu (sms) uliotumwa kutoka kwa simu mhanga.

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa kutoa taarifa za ndugu yake aitwaye Dickson Peter Mungulu kutekwa baada ya kupokea ujumbe mfupi simu uliotumwa kutoka kwa simu mhanga.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Justine Masejo amesema Julai 25 mwaka huu  majira ya saa 9:25 mchana  walipokea taarifa kutoka kwa mtu huyo  kuwa amepokea  ujumbe kutoka kwenye simu ya mhanga  ulioeleza kuwa ametekwa  na sharti la kuachiwa kitolewe kiasi cha Sh3 milioni ili aachiwe vinginevyo atauawa.

“Baada ya kupokea taarifa hizo Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi wa kina  na Julai 28, 2021 Jeshi la Polisi lilifanikiwa  kumpata kijana huyo aliyesadikiwa kutekwa maeneo ya Morombo  katika nyumba ya kulala wageni,”amesema Kamanda Masejo.

Kamanda Masejo amesema baada ya kumhoji Dickson Peter Mungulu ambaye mwaka 2020  alihitimu Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Makumira kilichopo wilayani Arumeru  ilibainika kuwa alitoa taarifa  za uongo kwa ndugu zake ili apate fedha hizo kumsaidia kulipa madeni yanayomkabili.

Msomi asingizia kutekwa baada ya kuelemewa na madeni


Amesema baada ya kumchunguza zaidi katika mwili wake ilibainika kuwepo kwa majeraha sehemu ya shingo  na mguu na alikiri kujichoma  na kitu chenye ncha kali yeye mwenyewe kwa nia ya kuwaaminisha wazazi wake kuwa alitekwa.

Kamanda Masejo amesema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na pindi uchunguzi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria.

“Natoa wito kwa wananchi  na vijana wenye tabia kama hii iliyooneshwa na kijana huyu kuwa jeshi la polisi halitawafumbia macho wale wote watakaohusika na litawachukulia hatua  kali za kisheria kwa watakaobainika kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uzushi ,”amesema Kamanda Masenjo.