Adaiwa kuvamia eneo la makaburi, apanda mahindi
Eneo la makaburi linalolalamikiwa na wananchi wa Mtaa wa Mangamba Juu likiwa limepandwa mahindi. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mangamba Juu, Manispaa ya Mtwara wameiomba Serikali kuingilia kati suala la mtu aliyedaiwa kuvamia eneo la makaburi na kuligeuza kuwa shamba.
Mtwara. Mtu aliyetambuliwa kwa jina la Mohamed Chando amedaiwa kujimilikisha eneo la makaburi ya wananchi wa Mtaa wa Mangamba Juu na kupanda mahindi .
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu, Chando amekanusha madai hayo akisema atakutana na Mtendaji wa Mtaa wa Mangamba Juu kisha atatoa mrejesho.
“Nipo kwenye kikao, lakini lalamiko hilo sio la kweli, tutakaa kikao na mtendaji kisha utapata mrejesho kuhusu suala hilo,” amesema Chando alipozungumza na Mwananchi.
Hata hivyo, Issa Rashidi Chipeto anayedai kuwa mmiliki wa eneo hilo amesema kuwa aliuza kipande na kuacha eneo la makaburi.
“Eneo lilikuwa la familia yetu hata kuuza niliuza mimi kwa kuwa baba amefariki na sikuuza eneo la makaburi kwa kuwa lilikuwa limesimamishwa uzikaji na lilikuwa na mgogoro.
“Nilipokuta uendelezaji unafanyika nilikwenda kuhoji kwa nini anaendeleza eneo hilo la makaburi na tena lilikuwa limekewa uzio kabisa,”amesema Chipeto.
Filemon Lilema aliyemzika baba yake katika eneo hilo mwaka 1992 ameeleza kusikitishwa na uvamizi huo.
“Nilitembelea kaburi la baba yangu mwaka 2019 nikakuta eneo limezuiliwa na linamilikiwa na mtu hadi nyumba imejengwa na kuna dada nilimwona akiishi hapo, lakini nilikwenda kudhuru kaburi la mzee nikaondoka,”amesema Lilema.
Amesema aliporudi mwaka 2023 alikakuta kuna pumba za kuku zimetunzwa juu ya kaburi, kuashiria kuwa kuna makazi ya watu eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi, aliyekuwa Mwenyekiti Kamati ya Urasimishaji wa maeneo hayo, Dominic Mpili amesema kuwa wakati wanaanza urasimishaji wa eneo la Mangamba Juu walifuata mipaka ya asili.
“Wakati wa urasimishaji tulikuwa tunaangalia mipaka ya asili, tulikuwa tukikuta kaburi tunaacha, lakini cha ajabu kuna mtu amevamia na hati anayo hata ramani yetu inaonyesha kuwa pale ni makaburi, lakini anasema kuwa ni lake” amesema Mpili.
Mpili amesema katika eneo hilo pia walimzika mdogo wake.
“Hatukujengea lile kaburi kutokana na kuvurugwa hakuna hata alama ya kuonyesha wapi tulimzika ndugu yetu huwezi kutambua, kibaya zaidi anafanya shughuli za kilimo ambapo ukimuuliza anajibu kibabe,” amesema Mpili.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mangamba juu, Nassoro Mtando amesema kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa watu waliozika ndugu zao, wakidai makaburi yamevunjwa.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mipango Miji Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mariam Kimolo amesema atafuatilia suala hilo ili kujua mmiliki halali wa eneo hilo.
"Nitakwenda kujiridhisha nijue kama ana hati nifahamu mipaka yake na nijue kiwanja namba ngapi kisha nitatoa jibu," amesema Kimolo.