Adakwa akisafirisha na dawa za kulevya

Muktasari:

 

Wakili wa Serikali, Matarasa Maharagande amedai  mbele ya Hakimu Adelf Sachore kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 26, mwaka huu eneo la nyumba za NSSF , wilaya ya Ilala.


Dar es Salaam. Mkazi wa Tabata, Linna Muro(44), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kujibu  shitaka la kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya heroin.

Wakili wa Serikali, Matarasa Maharagande amedai  mbele ya Hakimu Adelf Sachore kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 26, mwaka huu eneo la nyumba za NSSF , wilaya ya Ilala.

Maharagande amesema  kuwa  mshitakiwa alikutwa na kosa la kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 43.9.

Mshitakiwa alikana shitaka hilo ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Sachore, amesema mshitakiwa arudishwe rumande    ili ajiridhishe  kama shtaka linalomkabili linaweza kudhaminiwa au la.

Wakati huohuo, mfanyabiashara, Steven Almas (18), amefikishwa katika Mahakama hiyo kujibu shtaka la  unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi.

Mshtakiwa  amefikishwa mahakamani hapo na kupandishwa kizimbani leo , mbele ya Hakimu Mkazi Wilberforce Luhwago ambapo alisomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali Jacqueline Warema.

Werema  amedai mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 26, 2017 eneo la Chanika wilayani Ilala.

Inadaiwa siku ya tukio katika eneo hilo, mshitakiwa aliiba simu aina ya Samsung note3 yenye thamani ya Sh. 500,000 na fedha taslimu  Sh90,000,  vitu vyote vikiwa na  thamani ya Sh. 590,000, mali ya Sharif Halfan.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa kabla na baada ya wizi huo mshtakiwa alimjeruhi mlalamikaji kwa kumpiga rungu  kichwani ili kujipatia mali hizo.

Mshtakiwa alikana shitaka hilo na hakimu Luhwago ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 19,mwaka huu itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shauri linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.