Afa maji akivua samaki mtoni Lindi

Liwale. Hamis Nyihila (30), mkazi wa Kibutuka amefariki dunia akivua samaki katika mto Mbwemkuru, wilayani Liwale, mkoani Lindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Makuri amethibitisha uwepo wa tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi jana, kaka wa marehemu, Faraji Nyihila alisema Machi 15, 2024 saa 4.30 asubuhi aligundua mdogo wake amefariki dunia baada ya kukuta amezama majini katika mto Mbwemkulu.

Faraji ambaye ni diwani wa Kata ya Kibutuka, alisema mdogo wake alitoka nyumbani kwake Machi 3, 2024 saa nne asubuhi kwenda mtoni kuvua samaki, hakurudi hadi Machi 15, alipopatikana akiwa amefariki dunia.

"Mdogo wangu kazi zake ni uvuvi na kila siku huenda kuvua samaki katika mto huo, ametoka asubuhi ameenda kuvua lakini hadi jioni hakurudi. Ilibidi tutoke siku iliyofuata kwenda kumtafuta hakupatikana hadi Machi 15 alipopatikana akiwa amefariki dunia," alisema Faraji.

Mganga Mfawaidhi wa Kituo cha Afya Kibutuka, Dk Yohane Duway aliliambia Mwananchi kuwa baada ya uchunguzi wa mwili, walibaini sababu ya kifo ni kunywa maji mengi yaliyoingia kwenye mfumo wa hewa.

"Kifo cha Hamis kimetusikitisha, alikuwa mtu mwenye upendo na watu. Niwaombe wavuvi wawe makini kipindi hiki cha mvua, wachukue tahadhari mapema," alisema Fatuma Saidi ambaye ni jirani wa Hamis.

Matukio ya watu kufa maji yamekuwa yakijirudia mara kwa mara mkoani Lindi.

Desemba 30, 2023 katika eneo la pwani ya Kijiweni katika Manispaa ya Lindi, mtu mmoja alifariki dunia baada ya kunywa maji mengi na kushindwa kuogelea.

Tukio lingine lilitokea Januari 22, 2024 eneo la pwani la Mikumbi, ambako mtu mmoja alifariki dunia baada ya kunywa maji alipokuwa akivua samaki katika Bahari ya Hindi.