Afrika yajipanga uzalishaji wa chakula

Afrika yajipanga uzalishaji wa chakula

Muktasari:

  • Mkutano wa 39 wa kawaida wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika (UN), umefunguliwa leo Alhamisi Oktoba 14, 2021 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Addis Ababa. Mkutano wa 39 wa kawaida wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika (UN), umefunguliwa leo Alhamisi Oktoba 14, 2021 jijini Addis Ababa, Ethiopia.


Pamoja na mambo mengine, mawaziri hao watapitia andiko na mikakati ya utekelezaji wa kauli mbiu ya Mwaka 2022 ya “Lishe na Usalama wa Chakula barani Afrika.”


Kauli mbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa lishe bora kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa watoto barani Afrika, bara ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula.    


Hivyo, nchi za Afrika zinashauriwa kutekeleza mapendekezo ya Programu ya Afrika ya Maendeleo ya Kilimo na Azimio la Malabo, kuhusu kilimo ili kuondokana na changamoto ya lishe duni.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula anaongoza ujumbe wa Watanzania katika mkutano huo na katika mijadala yake, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika.


Balozi Mulamula atasisitiza suala hilo kwa sababu limeainishwa katika kauli mbiu ya mwaka 2021 ambayo imehimiza matumizi ya lugha za Kiafrika na Kiswahili ni moja ya lugha hizo ambayo inakuwa kwa kasi na kuzungumzwa na watu wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.


Aidha, katika mkutano huo, mawaziri watapokea taarifa kuhusu ugonjwa wa Uviko-19.


Katika hotuba ya ufunguzi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Christopher Litungula Apala, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuzingatia tahadhari za maambukizo ya Uviko ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu wao kupata chanjo ya ugonjwa huo.


Lakini pia alisisitiza jitihada ziendelea kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata idadi ya kutosha ya chanjo kwa ajili ya watu wake.
Katika Mkutano huo pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje watapitia na kupitisha bajeti ya Mwaka 2022 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi.


Nafasi hizo ni pamoja na za makamishna wawili wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Pan Africa, wajumbe wanne wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na wajumbe wanne wa Bodi ya Ushauri ya Afrika ya Kupambana na Rushwa.  


Pia, Mkutano wa 39 wa Mawaziri utapitia na kupitisha miundo ya taasisi saba za Umoja wa Afrika, ukiwemo muundo wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambalo Tanzania imeridhia Mkataba wake hivi karibuni. Kupitishwa kwa miundo hiyo itakuwa ni fursa zikiwemo za ajira kwa nchi wanachama.


Waziri Mulamula ametoa wito kwa  Watanzania kuzichangamkia nafsi hizo mara zitakapotangazwa.