Afrika yapoteza Dola 350 milioni kila mwaka utakatishaji fedha

Muktasari:

  • Nchi za Afrika hupoteza zaidi ya Dola 350 milioni kila mwaka kupitia utakatishaji fedha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof Florence Luoga amesema.

  

Arusha. Nchi za Afrika hupoteza zaidi ya Dola 350 milioni kila mwaka kupitia utakatishaji fedha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof Florence Luoga amesema.

Ametoa kauli hiyo imetolewa leo Juni 23, 2022 wakati akizungumza katika mkutano wa 10 ulioandaliwa na BoT na Jumuiya ya Kimataifa ya huduma Jumuishi za Fedha (AFI).

Mkutano huo ulioshirikisha viongozi wa jumuiya hiyo ukanda wa Afrika (AfPI) unaofanyika jijini Arusha.

Prof Luoga ambaye pia mwenyekiti wa AfPI amesema suala la utakatishaji wa fedha limeathiri nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Amesema nchi hizo zingechukua hatua za kudhibiti utakatishaji fedha, upotevu huo ungeweza kushuka hadi Dola 10 bilioni kwa mwaka.

Mkutano huo umeshirikisha magavana, manaibu magavana, wakuu wa taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha pamoja na watunga sera kutoka taasisi wanachama 32 kutoka nchi 30.

Kwa miaka miwili iliyopita, mkutano huo haukuweza kufanyika kutokana na janga la Uviko-19. Utajadili utoaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao na kuona iwapo zinaleta athari kwa wananchi pamoja na kubadilishana uzoefu na kupata ufumbuzi wa pamoja wa huduma ya teknolojia.

Amesema BoT imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wananpata huduma za kifedha umbali usiozidi kilomita 15 ili kuhakikisha huduma za kifedha zinabadili maisha ya wananchi.

Akifungua mkutano huo kwa njia ya mtandao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu imechangia kuongezeka kwa pato la taifa kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 66 mwaka jana.

Amesema hadi kufikia Desemba mwaka jana watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu walifikia milioni 35.3, sawa na asilimia 61 ya watu wote nchini.

"Kuanzishwa kwa huduma hizi za kifedha kwa njia ya simu pamoja na huduma za benki kwa wakala na benki kwa njia ya simu kuliongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini,"amesema.

Washiriki wa mkutano huo pia watajadili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuifanya sekta hiyo kuwa ya kidijitali zaidi barani Afrika na kukuza ushirikishwaji wa kifedha na maendeleo ya kiuchumi.

Alisema hali hiyo itasaidia kudhibiti ufisaidi, kuongeza uwazi na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AfPI, Dk Alfred Hannig amesema tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo mwaka 2013 msingi wake ni kusaidia maendeleo ya sera za huduma jumuishi na mipango ya udhibiti.