Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afukuzwa kazi akidai kucheleweshewa posho, mahakama yampa nafasi kupinga

Muktasari:

  • Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe imempa muda wa siku 14 aliyekuwa Ofisa Sheria Daraja la Kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Lusajo Mwakasege, kuwasilisha maombi ya mapitio akipinga kufukuzwa kazi, ambapo amedai alifukuzwa kazi kutokana na utoro uliosababishwa na kutokulipwa posho za uhamisho.



Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe imempa siku 14 aliyekuwa Ofisa Sheria Daraja la Kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Lusajo Mwakasege, kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa kufukuzwa kazi.

Mwakasege alifukuzwa kazi kwa kosa la kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano za kazi, lakini anadai utoro huo ulitokana na kucheleweshwa kulipwa posho zake za uhamisho baada ya kuhamishiwa kituo kipya cha kazi.

Uamuzi huo ulitolewa Julai 23, 2026 na Jaji Victoria Nongwa, aliyekuwa akisikiliza maombi ya Mwakasege dhidi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Tume ya Utumishi wa Umma, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika uamuzi wake, Jaji Nongwa alisema baada ya kupitia hoja za pande zote, Mahakama imejiridhisha kuwa Mwakasege ana maslahi ya kutosha katika suala linalohusu ajira yake na kwamba amewasilisha hoja zinazostahili kusikilizwa katika maombi ya mapitio ya kimahakama.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilimpa siku 14 kuwasilisha maombi hayo.

Kwa mujibu wa nyaraka za kesi, Mwakasege alihamishwa Februari 22, 2019 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Anadai baada ya kuhamishwa hakulipwa posho za uhamisho kwa wakati, hali iliyochangia kushindwa kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.

Badala ya suala hilo kushughulikiwa kama madai ya malipo ya posho, kutokuwepo kwake kazini kuligeuzwa kuwa shauri la kinidhamu.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Julai 3, 2019 alipewa notisi ya mashtaka ya kinidhamu kwa kosa la kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano za kazi, huku notisi hiyo ikimfikia Septemba 17, 2019.

Baada ya kujibu tuhuma hizo na kushiriki hatua za awali za mchakato wa kinidhamu, aliarifiwa kupitia barua ya Novemba 5, 2019 kuwa ajira yake ilikuwa imesitishwa kuanzia Oktoba 25, 2019.

Hakukubaliana na uamuzi huo na alikata rufaa, lakini rufaa yake ilikataliwa na uamuzi wa kufukuzwa kazi ukaendelea kusimama.

Aliendelea kutumia ngazi nyingine za rufaa za kiutawala, lakini hakufanikiwa kubadili uamuzi huo.

Mahakama ilieleza kuwa kupitia barua ya Aprili 19, 2022, ambayo ilitumwa tena kwake Aprili 9, 2025, Mwakasege aliarifiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa amethibitisha uamuzi wa kufukuzwa kwake Machi 26, 2022.

Baada ya kumaliza hatua zote za kiutawala bila mafanikio, alifungua shauri Mahakama Kuu akiomba apewe ruhusa ya kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama.


Hoja za Mwakasege

Katika maombi yake, Mwakasege anadai mchakato uliotumika kumfukuza ulikuwa na kasoro za kisheria na kiutaratibu.

Anadai hakufanyiwa uchunguzi wa awali uliokuwa wa lazima kabla ya kuanzishwa kwa hatua za kinidhamu.

Pia, anadai hakupata fursa ya kusikilizwa kikamilifu, hakualikwa kutoa maoni kuhusu ripoti ya kamati ya uchunguzi kabla ya uamuzi wa mwisho kufanywa, na hakuruhusiwa kuwasilisha hoja za kupunguza uzito wa kosa alilokuwa akituhumiwa.

Aidha, anadai uamuzi wa rufaa yake ulitolewa nje ya muda wa kisheria wa siku 90.


Mahakama ilivyoamua

Katika uamuzi wake, Jaji Nongwa amesema katika hatua ya kuomba ruhusa ya kufungua maombi ya mapitio ya kimahakama, mwombaji hahitajiki kuthibitisha madai yake yote, bali kuonyesha kuwa ana hoja zinazoweza kujadiliwa na Mahakama.

Amesema Mahakama imebaini kuwa madai ya Mwakasege kuhusu kutofanyika kwa uchunguzi wa awali, kutopata nafasi ya kusikilizwa, kutokushirikishwa katika hatua za uchunguzi na madai mengine ya ukiukwaji wa taratibu za kinidhamu yanastahili kuchunguzwa katika usikilizwaji wa shauri kuu.

"Kwa kuzingatia malalamiko hayo yote, bila kujali uhalali wake katika hatua hii, ninaridhika kuwa mwombaji ameonyesha kuwa ana kesi inayoweza kujadiliwa katika maombi yake ya msingi ya amri za certiorari na mandamus," amesema Jaji Nongwa.

Jaji huyo ameongeza kuwa Mwakasege alikuwa ametumia njia zote za kiutawala zilizokuwa wazi kwake, ikiwamo kukata rufaa katika mamlaka husika, hivyo maombi ya mapitio ya kimahakama ndiyo njia iliyobaki kwake kupinga uamuzi wa kufukuzwa kazi.

"Katika mazingira hayo, mahakama inaridhika kuwa mwombaji amekidhi vigezo vya kupewa ruhusa ya kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama," amesema.