Afutiwa kesi ya meno ya tembo, akaa mahabusu miaka sita

Dar es Salaam. Mkazi wa Kiwalani, Abubakar Mzava amefutiwa kesi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuahirishwa mara sita bila ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi, upande wa mashtaka huku akikaa mahabusu kwa muda wa miaka sita.

Mzava alikuwa anakabiliwa na kosa la kukutwa na vipande vitatu vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh34, 140,000.

Hata hivyo kesi hiyo inafutwa upande wa mashtaka waliieleza mahakama hiyo kuwa shauri limekuja kwa ajili ya kufanya makubaliano ya kumaliza kesi hiyo lakini mshtakiwa huyo alikana kuwa hajawasilisha  barua ya kuomba kumaliza shauri hilo.

Uamuzi huo umetolewa leo Mei 16, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate baada ya upande wa mashtaka kuahirisha mara sita na leo hii ni ya saba tangu mshtakiwa huyo asomewe hoja ya awali.

"Naona upande wa Jamhuri mmekuwa mkipoteza muda mkidai mnakaa na mshitakiwa kwa ajili ya mazungumzo ya pre bagain, kwa hiyo mimi leo naifuta kesi hii chini ya kifungu cha 225(5) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai," amesema Kabate.

 Alisema kesi hiyo tangu iliposomwa maelezo ya awali ilitakiwa ianze kusikilizwa lakini upande wa mashtaka walikuja na hoja kuwa wanafanya mazungumzo na mshtakiwa ili kumaliza kesi hiyo.

Hakimu Kabate alimtaka mshitakiwa huyo aeleze usahihi wa jambo hilo kwa sababu alishawahi kukanusha kuandika barua ya kutaka kufanya makubaliano ya kukiri shtaka hilo na kukutana na upande wa mashitaka kwa ajili ya mazungumzo.

“…naomba utuondolee huu utata uliopo wewe mwenyewe mshtakiwa,” amehoji Hakimu Kabate.

“Mheshimiwa tarehe iliyopita mawakili hawa hawa waliniuliza kuhusiana kufanya mazungumzo ili nimalize shauri hili, niliwaambia sijawahi kuandika barua yeyote…hata nakala ingeonekana, kilichokuwepo wanachelewesha kesi; mimi nipo mahabusu tangu mwaka 2018,” amejibu Mzava.

Baada ya maelezo hayo hakimu Kabate amesema kwakuwa upande wa mashtaka walioanzisha hoja hiyo, huku mshitakiwa akikana kukaa meza ya mazungumzo, ili kumaliza kesi hiyo, hivyo kwa mamlaka aliyopewa, alifuta kesi hiyo, kitendo kilichomuweka mtuhumiwa huru.