Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Agizo la RC Mtambi latekelezwa

Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi akiongea yalipo machimbo ya dhahabu katika Kijiji cha Chirorwe wilayani Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Kanali Mtambi alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho cha Chirorwe wakati alipokuwa akisikiliza  na kutatua kero za wakazi wa kijiji hicho sambamba na wachimbaji wadogo wa dhahabu.

Musoma. Kampuni ya Wakazi Mining inayomiliki leseni ya uchimbaji madini katika Kijiji cha Chirorwe, Wilaya ya Musoma mkoani Mara, imeilipa familia ya Ruhumbika Machumu fidia ya Sh40 milioni ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika eneo hilo.

Mbali na fidia hiyo, kampuni hiyo pia imelipia kodi ya pango la nyumba kwa miezi sita na kutoa Sh3 milioni kama fedha ya usumbufu ili kuiwezesha familia hiyo kuhama kutoka makazi yao ya awali.

Malipo hayo yamefanyika kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alilolitoa jana Julai 22, 2026, akiitaka kampuni hiyo kulipa fidia ndani ya siku moja ili kuondoa mgogoro uliokuwa ukikwamisha shughuli za uchimbaji na kuhatarisha usalama wa familia hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Chirorwe wilayani Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Julai 23, 2026, Kanali Mtambi amesema agizo hilo limetekelezwa kwa wakati na familia hiyo tayari imehama kupisha shughuli za uchimbaji.

Amesema shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu zinatarajiwa kurejea baada ya kusimamishwa kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ziara yake wilayani Musoma.

"Tayari hiyo Sh40 milioni imelipwa. Pia wamemlipia bibi kodi ya nyumba ya miezi sita pamoja na Sh3 milioni za usumbufu. Walihama usiku baada ya ule mkutano kama nilivyoagiza na wamefurahia walipopangishiwa," amesema Kanali Mtambi.

Mgogoro huo ulipata sura mpya Julai 4, 2026, baada ya familia ya Ruhumbika kuwasilisha kero yao kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakimuomba kuingilia kati mgogoro uliokuwa ukiendelea kati yao na wachimbaji wadogo. Baada ya kupokea malalamiko hayo, Dk Mwigulu aliamuru shughuli za uchimbaji kusitishwa kwa muda na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Mara kutafuta suluhisho la kudumu.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Damian Nyantora alisema awali walikubaliana kuilipa familia hiyo Sh40 milioni na kuwatafutia nyumba, lakini familia ilibadili msimamo na kudai Sh95 milioni. Kwa upande wake, msemaji wa familia hiyo, Sefaret Ruhumbika, alisema baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Serikali, familia imekubali kupokea Sh40 milioni kwa fidia ya ekari mbili na nyumba mbili ili kumaliza mgogoro uliodumu zaidi ya miaka miwili na kupisha shughuli za uchimbaji kuendelea.