Ahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kusafirisha bangi
Muktasari:
- Said Nayopa (30), mkazi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri makosa mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara.
Mtwara. Mahakama ya Wilaya ya Mtwara imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Said Nayopa (30), mkazi wa Kijiji cha Nambunga, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Katika shauri la jinai namba 13535 la mwaka 2026, mshtakiwa huyo alikabiliwa na makosa mawili ambayo ni kukutwa na kete 53 za bangi zenye uzito wa gramu 56 na kuhifadhi bangi kwenye mfuko wa plastiki angavu yenye uzito wa gramu 163.70.
Makosa hayo yote ni kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 95, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Awali, akisoma mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Mtwara, George Mbago, alieleza kuwa Mei 31, 2026, katika Kijiji cha Nambunga, Kata ya Hinju, mshtakiwa huyo alikutwa akiwa na kete 53 za bangi pamoja na kiasi kingine cha bangi kilichokuwa kimehifadhiwa kwenye mfuko wa plastiki angavu.
Mshtakiwa, baada ya kusomewa mashtaka yote mawili, alikiri makosa yake.
Aidha, mshtakiwa huyo alikiri maelezo yote yaliyotolewa mahakamani dhidi yake na yaliyosomwa na upande wa Jamhuri, uliowakilishwa na mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Thimosius Sulusi.
Baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kwanza na miaka mingine 30 kwa kosa la pili.
Hata hivyo, Mahakama iliamuru adhabu hizo zitumikiwe kwa pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha jumla cha miaka 30 jela.
Mshtakiwa alijitetea kwa kuiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa maelezo kwamba hilo lilikuwa kosa lake la kwanza.
Mahakama ilieleza kuwa adhabu hiyo inalenga kuwa fundisho kwa vijana wengine wanaojihusisha na matumizi na biashara za dawa za kulevya.
Hata hivyo, Mahakama imempa mshtakiwa siku 30 za kukata rufaa endapo hajaridhika na hukumu hiyo.