Ahukumiwa miaka 180 akitekeleza maagizo ya mganga wa kienyeji

Juma Msemwa aliyejifunika uso akiwa chini ya ulinzi wa Polisi katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe.
Muktasari:
- Juma amekumbana na hatia hiyo makosa sita ikiwemo kubaka na kulawiti pamoja na kuwalipa fidia ya Sh1 waathirika huku akiithibitishia Mahakama alitenda makossa hayo akitekeleza maagizo ya mganga wa kienyeji.
Njombe. Mahakama ya Wilaya ya Njombe imemhukumu Juma Msemwa (27) mkazi wa wilaya ya Njombe imemhukumu kutumika kifungo cha miaka 180 kwa kukutwa na hatia ya makosa sita yakiwemo matatu ya ubakaji na matatu ya ulawiti.
Akisoma hukumu hiyo shauri namba 53 la mwaka 2023 Hakimu Mkazi Wilaya ya Njombe, Matilda Kayombo amesema mshtakiwa huyo amekutwa na hatia katika makosa sita matatu yakiwa ni ubakaji na matatu mengine ni ulawiti.
Amesema makosa hayo anadaiwa kufanya Mei 16 hadi 23 mwaka huu katika mtaa wa Kihesa eneo la Kilimani mkoani Njombe.
Amesema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wakiwemo waathirika wa matukio.
"Taarifa ya uchunguzi wa daktari, uongozi wa Serikali ya mtaa na ushahidi wa Polisi, kijana Juma Msemwa anadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kwa kuwahadaa wanawake watatu na kisha kuwafungia katika nyumba aliyokuwa anaishi," amesema Kayombo.
Amesema mshtakiwa huyo alikuwa anaishi mtaa wa Kihesa ambapo aliwalawiti na kuwabaka kwa zamu wanawake hao zoezi ambalo lilienda sambamba na kuwaingiza magunzi ya mahindi na matango katika sehemu za siri.
Amesema taarifa hizo zilitolewa na mmoja kati ya wanawake aliokuwa amewateka na kufanikiwa kutoroka na kuomba msaada kwa majirani.
Amesema majirani hao walivamia nyumbani kwa mshtakiwa huyo na kukuta wanawake wawili wakiwa ndani huku kukiwa na mfuko wenye dawa za kienyeji.
Amesema sehemu ya ushahidi uliotolewa ulibainisha kuwa mshtakiwa huyo alikiri kuwa amefanya matukio hayo akiwa anatekeleza maagizo ya mganga aliyemtaka abake wanawake na watoto.
Amesema makosa aliyotenda mshtakiwa huyo ni kinyume na sheria kifungu namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (e) sambamba na kifungu kidogo cha sheria ya adhabu ya kifungu namba 16 kama ilivyofanyiwa marejeo 2022.
Amesema hukumu hiyo inakwenda sambamba na fidia ya fedha halali za Kitanzania Sh1 milioni kwa kila muathirika wa makosa aliyofanyiwa.
Naye mwendesha mashtaka wa Serikali, Magdalena Whero na Elise James waliiomba mahakama kutoa hukumu kali kwa mshtakiwa ili iwe funzo kwa jamii yote hasa ikizingatiwa kwamba matukio ya ubakaji na ulawiti yamekuwa yakiongezeka mkoani Njombe.