AI kusaidia ofisi za mawakili kupunguza mzigo wa kazi
Muktasari:
- MatterMiner ni mfumo utakaosaidia katika utozaji wa ada, ukiwa na usaidizi wa michakato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi nyingine.
Dar es Salaam. Teknolojia ya Akili Unde (AI) inaanza kubadili namna kampuni za uwakili zinavyosimamia mashauri, mapato na shughuli za kila siku, baada ya kampuni ya teknolojia ya sheria kutoka Marekani kuzindua mfumo maalumu unaolenga kuendana na mazingira ya kisheria ya Afrika.
Mfumo huo unaoitwa MatterMiner umezinduliwa na kampuni ya Mkenga Na Namwaka, Incorporated, ukiwa na lengo la kusaidia kampuni za uwakili kuondokana na mifumo inayotegemea kazi za mikono katika kusimamia shughuli zao.
Mfumo huo unaunganisha usimamizi wa mashauri, utozaji wa ada wenye usaidizi wa michakato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi nyingine, usimamizi wa akaunti za amana, kalenda, kazi na tarehe muhimu za mwisho, pamoja na ripoti na uchambuzi wa utendaji kwa ajili ya uongozi wa kampuni.
Mwanzilishi na Mmiliki wa Mkenga Na Namwaka, Incorporated, Elsante Mnzava, akizungumza leo Jumatatu, Julai 20, 2026, amesema kampuni hiyo imeanza utekelezaji wa mfumo huo barani Afrika baada ya kubaini kuwa kampuni nyingi za uwakili zinakabiliwa na changamoto zinazofanana katika uendeshaji wa shughuli zao.
Amesema changamoto hizo ni pamoja na kupoteza muda ambao ungeweza kutozwa ada, kupitwa na tarehe muhimu za mashauri, matumizi ya mifumo mingi isiyounganishwa, ugumu wa utozaji wa ada na usimamizi wa fedha za amana.
“Kwa zaidi ya muongo mmoja tumekuwa tukitoa suluhisho za teknolojia ya sheria, na tumeona kampuni za uwakili zikihitaji mifumo inayoakisi namna wanavyofanya kazi katika mazingira yao halisi, ikizingatia lugha, taratibu na mahitaji ya kila soko,” amesema Mnzava.
Amesema Akili Unde itakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya MatterMiner, lakini haitatumika kuchukua nafasi ya uamuzi wa wataalamu wa sheria, bali kusaidia kupunguza kazi zinazojirudia na kuongeza ufanisi.
“Wanasheria bado ndio wenye jukumu la kutoa uamuzi wa kitaalamu, mikakati na uwajibikaji kwa wateja wao. AI inalenga kuwa chombo cha kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Mkenga Na Namwaka, Incorporated, yenye makao makuu nchini Marekani, imesema MatterMiner imejengwa kutokana na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika teknolojia za sheria na utekelezaji wa zaidi ya miradi 250 kwa kampuni za uwakili duniani.
Mshirika Mkuu wa ADNA Law, Salimatou Diallo, amesema kampuni za uwakili zinahitaji teknolojia ya usimamizi wa shughuli za kisheria inayoakisi namna kazi za kisheria zinavyotekelezwa katika mazingira ya eneo husika.
“Hii inajumuisha taratibu za kazi, lugha, mifumo ya utawala na hali halisi za utekelezaji. Mfumo huu umeundwa kwa ajili ya washirika wenye hisa na washirika wasimamizi, viongozi wa uendeshaji, timu za fedha na wadau wa tehama katika kampuni za uwakili zilizoimarika na zinazokua,” amesema.