Aishi miaka 8 ubongo wazi, aomba matibabu

Marwa Msyomi akionyesha jeraha lililopo kichwani baada ya fuvu la kichwa chake kupasuliwa baada ya kushambuliwa alipoamulia ugomvi uliokuwa umetokea kijijini kwao, Rebu wilayani Tarime Desemba 2014. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Wema umemponza Marwa Msyomi (30) na kusababisha aishi kwa miaka mingi ubongo ukiwa nje ya fuvu baada ya kujeruhiwa kwa mapanga alipoamulia ugomvi mtaani kwake.

Wema umemponza Marwa Msyomi (30) na kusababisha aishi kwa miaka mingi ubongo ukiwa nje ya fuvu baada ya kujeruhiwa kwa mapanga alipoamulia ugomvi mtaani kwake.

Ingawa anapumua vizuri na anao uwezo wa kujieleza, harufu ya vidonda alivyonavyo hufika umbali mrefu kutoka alipo. Hali hii inaendelea licha ya juhudi za madaktari wa Hospitali ya Rufaa Bugando kujitahidi kumtibu kabla hawajamruhusu kwenda Hospitali ya Kanda KCMC kwa tiba za kitaalamu zaidi.

Aishi miaka 8 ubongo wazi, aomba matibabu

Marwa ameishi kwenye hali hii tangu Desemba 2014 alipoamulia ugomvi wa vijana wawili waliokuwa wanamshambulia mwenzao. Msaada huo ulimsaidia aliyekuwa anapigwa kupata upenyo wa kukimbia ndipo mahasimu wake walipohamishia hasira zao kwa Marwa.

Wallimkata kwa mapanga kichwani, fuvu lake likapasuka vibaya kiasi cha kukaa Hospitali ya Wilaya Musoma kwa wiki nzima bila kupata fahamu hali iliyowapa madaktari sababu ya kumruhusu ahamishiwe Hospitali ya Rufaa Bugando.

Baada ya matibabu yaliyodumu tangu Agosti 14 mwaka 2017 alipopewa rufaa ya kwenda KCMC, madaktari wameona inafaa sasa kwa majeruhi huyo kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) lakini kupata nauli ya kumfikisha jijini Dar es Salaam ukawa mtihani mkubwa kwake mpaka waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato la kijijini kwao Rebu huko wilayani Tarime walipomchangia ndipo Februari 21 aliingia katika Jiji la Makamba ili aende Muhimbili.

Safari ya kutoka mkoani Mara kupitia Mwanza kuja Dar es Salaam ilikuwa ngumu kwake, iliyojaa unyanyapaa kutokana na harufu kali inayotoka katika majeraha aliyonayo kichwani.

Mmoja wa abiria aliyesafiri na Marwa kutoka Musoma mpaka Dar es Salaam, Fortunatus Daniel anasema kuna mahali basi lilisimama ili abiria wachimbe dawa na kila mmoja akawa analalamika kwamba “kuna harufu kali inatoka upande wa nyuma ya gari” lakini kwa kuwa dereva alishapewa taarifa, akawatuliza.

Hata hivyo, abiria hao walikubaliana madirisha yabaki wazi muda wote. Waplipofika mkoani Dodona, Daniel anasema basi lao liliharibika hivyo akapata wasaa wa kwenda kuzungumza na Marwa aliyemsimulia mkasa uliompata.

“NIlipomaliza kuzungumza abiria wenzangu walitaka kujua nimeongea naye nini. Kwa hali aliyonayo walidhani hawezi kuzungumza. Anahitaji msaada wa haraka sana,” alisema Daniel.

Hakumwacha bure, Daniel alimshauri Marwa kulitafuta gazeti hili ili limsaidie kufikisha taarifa kwa Watanzania ambao wanaweza kumchangia matibabu ili apone na kuendelea na majukumu yake kama baba na mume.

“Ninawashukuru kwa kwenda kuongea naye. Marwa anapitia kipindi kigumu sana. Kuna wakati anashinda kujieleza, hajiamini na vile watu wanavyoiogopa harufu y akidonda chake, anakosa amani kabisa,” anasema Daniel, mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam lakini mwenyeji wa Musoma.


Chanzo cha majeraha

Marwa anasema Jumapili moja ya Desemba 2014 akiwa ametoka kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo, wakati anarejea nyumbani aliwaona vijana wawili wanampiga mwenzao hivyo akaingilia kuwaamua lakini akageuziwa kwa kuanza kushambuliwa yeye.

“Walinipiga mpaka nikapoteza fahamu…nilishtuka nikiwahospitalini nilikolazwa kwa wiki nzima,” anasema Marwa aliyekuwa anajishughulisha kwa kilimo huku akiendesha bodaboda.

Kutoka Hospitali ya Wilaya Tarime alikoanzia matibabu alihamishiwa Hospitali ya Wilaya Musoma kabla hajapewa rufaa kwenda Bugando halafu KCMC na sasa Muhimbili.

“Bugando walinipiga X-Ray wakaona fuvu limepasuka. Walinifanyia upasuaji wa kulitoa fuvu lililopasuka npakabaki wazi. Nilirudi nyumbani lakini lile eneo likawa linachezacheza kama utosi wa mtoto mdogo halafu napata maumivu,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anasema familia ilimrudisha tena Bugando ambako alitakiwa kuwekewa chuma kufunika hiyo sehemu ivyo gharama za matibabu yake zikaanza kuwa kubwa.

“Tulirudi nyumbani, tuliuza mali zote ndipo nikawekewa hicho chuma. Baada ya kufunika kidonda, nyuzi zilipoanza kukatika hakikushikana vizuri kikaanza kuachia mpaka hadi chuma kikaanza kuonekana. Hali imebaki hivyo, chuma kinaonekana,” anasema.

Kutokana na kuwa wazi, anasema kidonda hicho kinamsababishia magonjwa mengine ikiwamo degedege, kizunguzungu, kupooza upande wa kushoto, macho kutoona vizuri na maumivu makali ya kichwa.

Tangu alipopewa rufaa ya kwenda Muhimbili mwaka 2017, Marwa anasema hajapata matibabu yoyote mpaka sasa anapohangaika kukutana na watalamu wa Muhimbili.

“Sijawahi kutumia dawa yoyote kuosha kidonda wala kutuliza maumivu. Rufaa nilipewa mwaka 2017 lakini niliitunza ndani ili siku nikipata fedha nisafiri kuja Dar es Salaam kutibiwa. Jeraha kama unavyoliona, lipo wazi. Kuna wakati funza wanatoka na usaha pia. Nashindwa kukaa na watu kwa sababu ya harufu ya uvundo inayotoka,” anasema.


Aomba msaada

Mke wa Marwa, Jane Marwa Ghati anawaomba Watanzania kusaidia mumewe atibiwe. “Tuna maisha magumu sana kwani mimi ndiyo mama na baba. Tukiwa nyumbani, nauza ndizi ili tupate chochote. Nauli ya kufika huku tulichangiwa kanisani hata hela ya kula njiani ilikuwa shida.”

Kwa sasa, anasema wanaishi Ukonga Mombasa walikopata chumba ila wanalala chini kwani bado hawana godoro.

Ili kuchangia Marwa, unaweza kumtumia chochote katika namba 0747362904 iliyosajiliwa kwa jina Matinde Msyomi.