Ajali barabarani zaongezwa katika magonjwa yasiyoambukizwa

Muktasari:

Serikali imeongeza ajali za barabarani katika idara ya magonjwa yasiyoambukiza na Afya ya akili ili kutoa kipaumbeke katika bajeti ya Wizara ya Afya.

Dodoma. Serikali imeongeza matukio ya ajali katika Idara ya magonjwa yasiyoambukiza ili kuyapa kipaumbele katika bajeti yake.

Pia Serikali imeifanya kuwa Idara ya magonjwa yasiyoambukiza, ajali na Afya ya akili.

Hayo yamesemwa leo Novemba 14, 2022 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akitembelea majeruhi wa ajali ya basi la Arusha Express lililogangana uso kwa uso na lori la mchanga jana katika eneo la Zanka nje kidogo ya Jiji la Dodoma na kusababisha vifo vya watu saba.

Waziri Ummy amesema janga la ajali linakua kwa kasi, hivyo Serikali imetenga idara maalum itakayoshughulika na masuala ya majeruhi wa ajali hususan ajali za barabarani ambazo zinaigharimu Serikali katika matibabu yake.

Ummy amesema gharama za mgojwa mmoja anayepata ajali ambaye atafanyiwa upasuaji wa kawaida sio chini ya Sh150, 000 na majeruhi aliyeumia tumbo, kichwa au miguu sio chini ya Sh600, 000 na kwa atayehitaji kuwekewa vipandikizi (vyuma) atagharamia kiasi cha fedha sio chini ya Sh2 milioni.

"Sisi Wizara tunaelemewa na mzigo wa wagonjwa na majeruhi wa ajali za barabarani, kwa hiyo tumeongeza kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza na sasa kitakuwa ni Idara ya magonjwa yasiyoambukiza, ajali na Afya ya akili ili ajali nazo zipewe kipaumbele,” amesema Ummy.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Ibenzi Ernest amesema jana majira ya saa 7 mchana walipokea miili sita na majeruhi 22 wa ajali hiyo ambayo chanzo chake ilidaiwa kuwa ni kulipita gari lingine na kugongana uso kwa uso basi hilo.

Ibenzi amesema kati ya majeruhi hao 11 wanaendelea kupatiwa matibabu, 9 wameruhusiwa, mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa na mmoja alifariki dunia wakti akiendelea kupatiwa matibabu.