Ajali sasa tishio Mkoa wa Pwani

Muktasari:

Ajali nyingine ilitokea Rufiji Machi 26, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wawili wakitokea jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye gari dogo lililogongana na lori eneo la Nyamwage

Pwani/mikoani. Ajali za barabarani zim-eendelea kuutesa Mkoa wa Pwani, tatu zikitokea ndani ya siku nne na kusababisha vifo vya watu sita.

Miongoni mwa hizo ni ile iliyotokea asubuhi ya leo Machi 29, 2024 na kusaba-bisha vifo vya mashabiki wawili wa klabu ya soka ya Simba.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Vigwaza wilaya-ni Chalinze ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster lililobeba mashabiki wa Simba tawi la Kiwira, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya waliokuwa wakielekea Dar es Salaam kushuhudia mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly ya Misri na Simba iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo,  amesema gari hilo liligongana na lori na kusababisha vifo vya watu hao aki-wamo dereva wa Toyota Coaster, Moses Mwaisela na abiria Oleison Mwakasila.

Majeruhi katika ajali hiyo alisema ni Debo-ra Barton, Devota Mwantobe na Erasto Mwalisalite, wote wakazi wa Tukuyu, mkoani Mbeya wanaoendelea na matibabu katika Hospital ya Msoga wilayani Chalinze, mkoani Pwani.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mo-hamedi Shabani amekiri kupokea majeruhi hao ambao alisema hali zao zinaendelea vi-zuri

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amewajulia hali majeruhi hao na kutoa pole kwa familia za mashabiki waliofariki dunia.

Hii ni ajali ya tatu kutokea ndani ya siku nne katika mkoa huo, zikigharimu maisha ya watu sita na majeruhi sita, chanzo kikielezwa kuwa uzembe wa madereva.

Ajali nyingine ilitokea Rufiji Machi 26, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wawili wakitokea jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye gari dogo lililogongana na lori eneo la Nyamwage.

Nyingine ilitokea eneo la Ruvu, Machi 28, 2024 iliyosababisha vifo vya watu wawili na majeruhi watatu ikuhusisha mabasi mawili ya kampuni za Sauli na New Force ambayo yaliligonga lori ubavuni na baadaye kutokea mlipuko wa moto, uliosababisha magari hayo kuteketea.


Hatua zinazochukuliwa

Kutokana na mwendelezo wa matukio ya ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeweka mpangokazi wa muda mrefu wa kudhibiti ajali hizo,  ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa ma-dereva wa malori na mabasi.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa rai kwa madereva kuzingatia sheria za usala-ma barabarani na kuchukua tahadhari, pia kuwa na udereva wa kujihami muda wote ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukwa,” amesema Kamanda Lutumo.

Simulizi ajali ya Ruvu

Baadhi ya abiria, madereva wa mabasi, da-ladala na magari madogo walisimulia adha waliyopata baada ya ajali iliyosababisha foleni kubwa iliyoanzia Ruvu hadi Kongowe.

Kwa mujibu wa Kamanda Lutumo, hadi leo asubuhi bado magari yalikuwa mengi kwenye barabara hiyo, hasa malori yali-yokuwa yakitokea Dar es Salaam kwenda mikoani.

"Kikubwa ni madereva na abiria kuwa wavumilivu na wastaarabu barabarani, wapo wengine wanapenda kutanua na barabara zetu hizi ni nyembamba, hivyo tunawapa elimu kuendelea kuwa wavumili-vu," amesema.

Barabara hiyo ndiyo inaunganisha mawasiliano ya mikoa ya Dar es Salaam kupitia Pwani kwenda mikoa ya kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Mashariki, Maghari-bi na nchi za jirani.

Baadhi ya abiria wamesema juzi walilaz-imika kulala barabarani.

"Tulifika Ruvu saa 4.16 usiku barabara zote zimefungwa, hakuna gari linalotem-bea kuanzia zile za kutoka Dar es Salaam na zile zilizokuwa zikitokea njia ya Chalinze likiwamo basi letu," amesema Sophia Man-yama, aliyekuwa akitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

"Dereva alipenya-penya huko ndani-ndani, tukaja kutokea kwenye mataa ya Mlandizi, napo tukakuta barabara imefunga. Pale hatukutembea tena hadi saa 8 usiku, dereva akaamua kulizima gari, ikabidi tulale ndani ya gari,” amesema.

Askari wa usalama barabarani ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msema-ji, alisema saa tisa usiku wa kuamkia jana Machi ndipo kazi ya kuyaondoa magari yaliyopata ajali ilikamilika.

Abiria mwingine, Juma Haji ambaye amesema alipata shida ya kupata usafiri stendi kuu ya mabasi ya Msamvu mkoani  Morogoro ambako alisubiri kwa zaidi ya saa sita.

"Nimekata tiketi (analitaja mojawapo ya mabasi yanayofanya safari zake Dar-Morogoro) saa 5.16 asubuhi nikaambiwa niwe mvumilivu basi litakuja kwa kuwa mengi yapo kwenye foleni Kibaha.

"Pale stendi watu walikuwa wengi, kili-chotokea hatukuwa tunapanda basi kwa namba ya gari iliyopo kwenye tiketi, bali kwa herufi, tiketi yangu ilikuwa ni herufi L, wakati nafika stendi nilikuta abiria wa herufu E hawajapata basi," amesema.

Amesema hadi alipopata gari la herufi yake ilikuwa saa 12.21 jioni juzi na alifika Dar es Salaam saa 11.00 alfajiri ya jana.

Mmoja wa madereva wa gari ndogo, ali-yekuwa akitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam, Anthony Mathias alisema hajawahi kukutana na foleni kama hiyo.

"Nilizima gari, nikatafuta kikoi nikalala pembezoni mwa barabara hadi saa 9.30 us-iku ndipo magari yakaanza kusogea mdogo-mdogo, sitasahau siku hii, nimetumia ta-kribani saa 24 kutoka Dodoma kufika Dar es Salaam," amesema.

Dereva mwingine, Rajabu Shabani wa da-ladala inayofanya safari kati ya Chalinze na Dar es Salaam, amesema alilazimika kupenya njia za ndanindani baada ya kufika Vigwaza, lakini haikusaidia.

"Kule hakukuwa na foleni, lakini kuna nyakati unalazimika kurudi barabara kubwa, na safari inaishia hapo, siku ilikuwa ngumu kwenye muda hadi kibiashara, niombe Serikali yetu ingeona utaratibu wa kui-panua barabara hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Operesh-eni wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Nassoro Sisiwaya amepiga marufuku ma-gari mabovu kuingia barabarani, akiwataka madereva na wamiliki wa magari hayo kutii sheria ya usalama barabarani.

Sisiwaya amesema hayo leo Machi 29, 2024 mkoani Iringa wakati wa ukaguzi wa vyombo vya moto, akiwataka madereva na wamiliki wa magari kutii sheria za usalama barabarani na kuacha tabia ya kutumia yaliyo mabovu.

Amesema sheria haimtaki tu dereva bali pia mmiliki anatakiwa kuhakikisha chombo husika kinakuwa salama kwa watumiaji wengine kabla ya kuingia barabarani.

“Tupo Iringa tunaendelea na operesheni ya kukamata magari mabovu, mwendokasi, wanaokimbia kulipa madeni ya Serikali, namba za 3D, vimulimuli na ving'ora,” amesema.

“Katika operesheni hii baadhi ya magari tumeyazuia ili yatengenezwe na yataka-pokaguliwa ndipo yataruhusiwa kurudi barabarani,” amesema.

Awali, Kaimu Mkuu wa usalama barabara-ni Mkoa wa Iringa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Glory Mtui, alisisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu ili kutokomeza ajali mkoani humo.

Pia inalenga kujenga uelewa kwa ma-dereva na wamiliki wote wa vyombo hivyo vya moto.

Amesema magari mabovu hayaruhusiwi kuingia barabarani si kwa nyakati za siku-kuu pekee bali ni kwa nyakati zote pindi dereva anapotaka kuanza safari yake.

"Wakati wowote dereva anapoingiza gari barabarani anawajibu wa kuhakikisha kabla hajaanza safari anapaswa kufanya ukaguzi wa gari lake linakuwa katika ubora ambao unatakiwa." amesema.

Imeandikwa na Sanjito Msafiri (Pwani), Imani Makongoro (Dar) na Mary Sanyiwa (Iringa)