Ajali ya lori, Coaster yaua tisa Bagamoyo

Moja ya gari lililopata ajali na kusababisha vifo watu tisa Bagamoyo mkoani Pwani usiku wa Machi 10, Mwaka huu.

Muktasari:

  • Watu tisa wapoteza maisha katika ajali iliyotokea wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani baada  ya magari mawili kugongana uso kwa uso, chanzo kikitajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa lori lilokuwa limebeba mawe.

Bagamoyo. Watu tisa wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha magari mawili wilayani Bagamoyo Mkoa Pwani jana Machi 10, 2024 jioni.

Akizungumzia  tukio hilo  Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema taarifa za awali zinaonyesha kuwa dereva wa lori alikuwa anayapita magari yaliyokuwa mbele yake kwenye eneo lisiloruhusiwa, ndipo alipogongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Toyota Coaster.

"Ajali imetokea eneo la Kiromo Bagamoyo Mkoa wa Pwani na dereva wa lori aliyekuwa akitokea Bagamoyo kwenda Dar es Salaam alikuwa anayapita magari kwenye eneo lisiloruhusiwa, ndipo akagongana uso kwa uso na gari ya abiria aina ya Toyota Coaster iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Bagamoyo," amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema kuwa kati ya waliopoteza maisha, saba ni wanaume na wawili ni wanawake.

"Majeruhi watatu wamefikishwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya matibabu," amesema.

Amesema kuwa mpaka sasa hawajapata taarifa kuhusu dereva wa lori hilo aitwaye Apolo Isdori, mkazi wa Kibaha mkoani humo na kwamba wanaendelea na uchunguzi.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na wataendelea kutoa taarifa zaidi kadiri uchunguzi juu ya tukio hilo unavyoendelea.