VIDEO: Saa nne za kuopoa gari lililotumbukia ziwani Mwanza

Lori lililoopolewa baada ya kuzama ziwani

Muktasari:

  • Gari hilo lilitumbukia ziwani eneo la Kigongo wilayani Misungwi mkoani Mwanza Februari 28, 2024, saa 2:30 usiku baada ya kuteleza wakati linapakiwa ndani ya kivuko cha MV Sengerema.

Mwanza. Imechukua saa 4:30  kwa mashine ya kuinua  vitu vizito  ya mgodi wa madini Geita Gold Mine (GGM),  kuiopoa gari lililokuwa limetumbukia ndani ya Ziwa Victoria.

Gari hilo mali ya kampuni ya ujenzi ya Casco lilitumbukia  eneo la Kigongo wilayani Misungwi mkoani Mwanza Februari 28, 2024, saa 2:30 usiku baada ya kuteleza wakati linapakiwa ndani ya kivuko cha MV Sengerema kinachotoa huduma kati ya Kigongo na Busisi Sengerema.

Baada ya ajali hiyo kutokea, jitihada zilifanyika kwa kuleta kreni yenye uzito wa tani 60, hata hivyo haikufua dafu hadi ilipoletwa kreni ya GGM yenye uzito wa tani 140.

Akizungumza baada ya shughuli ya kunasua gari hilo, dereva wa gari hilo, Hashim Ezat ameleeza kufurahisha na jitihada zilizofanyika, huku akisema nafsi yake imeridhika na jitihada hizo.

"Namshukuru Mungu nilikuwa nawaza sana kuhusiana na hii gari, lakini Mungu ametenda imetolewa (imenasuliwa) salama na haina tatizo lolote pamoja na kukaa ziwani kwa siku mbili," amesema Ezat.

Saa nne za kuopoa gari lililotumbukia ziwani

Meneja wa vivuko Kanda ya Ziwa Magharibi, Vitalis Bilauli amesema shughuli hiyo imefanikiwa kwa asilimia 100 na tayari gari hilo limevushwa upande wa pili (Busisi) kwa ajili ya kuendelea na safari yake.

"Naomba kutoa taarifa njema kwa umma kwamba tumefanikiwa kuinasua gari iliyokuwa imetumbukia ziwani. Hatuna tukio lolote la mtu kuumia au kufariki na chombo tumekifanyia majaribio na mambo yako vizuri huduma zimerejea kama kawaida. Tunawashukuru sana GGM kwa msaada wao," amesema Bilauli.

Hata hivyo, Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli (Tasac), Rashid Katonga amesema baada ya kufanya ukaguzi wa kivuko kilichokuwa kimebeba gari hilo, wamebaini hakijapata athari yoyote na kimeanza kutoa huduma katika eneo hilo.

Pia amesema ajali hiyo haijaleta athari za kimazingira na miundombinu,  huku akiwataka wakazi wa Kanda ya Ziwa wanaotegemea huduma ya kuvuka eneo hilo kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkazi wa Sengerema mkoani humo, Elizabeth Mussa ambaye alikuwepo wakati wa uopoaji  wa gari hilo,  ameishauri Serikali, kuweka kreni maeneo yenye miundombinu ya namna hiyo ili kupambana na changamoto za aina hiyo zinapojitokeza.