Lori latumbukia ziwani likiingia kwenye kivuko

Hashim Ezat, dereva wa lori lililotumbukia Ziwa Victoria, eneo la Kigongo wilayani Misungwi mkoani Mwanza juzi Februari 28, 2024. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Hakuna madhara kwa binadamu, jitihada za kulinasua zaendelea

Mwanza. Lori lililopakiwa kwenye kivuko kwa ajili ya kuvushwa kutoka Kigongo wilayani Misungwi kwenda Busisi, Sengerema limetumbukia ziwani.

Lilikuwa limepakiwa kwenye kivuko cha MV Sengerema kinachofanya safari ndani ya Ziwa Victoria kati ya Kigongo kwenda Busisi, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Taarifa ya tukio hilo imethibishwa leo Ijumaa Machi mosi, 2024 na Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa Magharibi, Vitalis Bilauli.

Amesema ajali hiyo ilitokea Februari 28, mwaka huu saa 2.30 usiku.

Bilauli  amesema gari lenye mtambo wa uchimbaji lililokuwa limeshaingia kwenye kivuko lilianza kurudi nyuma na kusababisha kivuko kusogea majini kutoka kwenye gati la kupakilia abiria na magari.

Amesema hakuna athari zilizojitokeza kwa binadamu wala magari mengine.

Bilauli  amesema jitihada za kulinasua gari hilo zilikwama, jambo lililowalazimu kuagiza kreni kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

"Tulikuwa tunapandisha magari kwenye kivuko sasa hilo gari lilivyoingia kwenye kivuko baadaye dereva sijui alijisahau akaanza kurudi reverse (nyuma) lilivyogusa ardhi wakati upande wa mbele uko kwenye kivuko ndiyo likakisukuma kwenda mbele likawa limening'inia nusu majini na nusu kwenye kivuko,” amesema.

"Gari lililonasa hapa ni tani 43 na mitambo ambayo tumeileta tangu jana imefeli, kwa hiyo tumefanya jitihada tumeagiza mtambo mkubwa kama tani 140 ili tulinasue. Hakuna hasara wala mtu aliyeumia kutokana na ajali hii, tunaendelea na uvushaji wa abiria kama kawaida," amesema Bilauli.

"Katika upandishaji, huwa tunaanza na magari, wanafuata abiria sasa tulikuwa tumeshapakia magari kama matano ndipo likatokea hilo na abiria wakawa wamekwama kuingia," amesema.

Bilauli amesema wananchi wanaendelea kupatiwa huduma na vivuko vingine viwili ambavyo vina uwezo wa kubeba abiria 1,000 na magari 24 kila kimoja. Vivuko hivyo ni MV Mwanza na MV Misungwi.

Akieleza tukio hilo, dereva wa gari lililotumbukia, Hashim Ezat amesema alipoanza kuingia ndani ya kivuko mbele kulikuwa na lori lingine lililomzuia kuingia ndipo alipojaribu kurudi nyuma ili kupata nafasi, lori lilianza kusukuma kivuko kwenda ziwani hatimaye gari lake likatumbukia majini.

"Bahati nzuri halikutumbukia lote, hivyo nilipata upenyo wa kutoka bila madhara wala hakuna mtu aliyejeruhiwa. Tunaendelea na jitihada za kulinasua, tangu juzi tumetumia kreni zinazofanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa daraja la JPM zimeshindwa, lakini wamesema kuna kreni  inatoka GGM," amesema Ezat.

Mkazi wa Geita, Mariam Maduhu amesema kutokana na ajali hiyo vivuko vinavyotoa huduma vimebaki viwili, hivyo ameomba kinasuliwe ili kuongeza ufanisi wa abiria kuvuka eneo hilo.