Sintofahamu kusitishwa huduma za kivuko Kigamboni

Muktasari:

  •  Kusitishwa kwa huduma za kivuko cha MV Kigamboni kunasababisha wenye magari wanaotaka kuingia au kutoka Kigamboni kulazimika kuzunguka njia ya Daraja la Mwalimu

Dar es Salaam. Wakazi wa Kigamboni wametoa kilio chao kufuatia kuendelea kuzorota kwa huduma za vivuko kati ya Kigamboni na Magogoni, huku wakiitaka Serikali ichukue hatua kupata suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Kilio hiki kimekuja kufuatia taarifa ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) kuhusu kusitishwa kwa huduma za kivuko cha MV Kigamboni kuanzia alfajiri ya leo Jumamosi Janauri 27, 2024, kutokana na hitilafu ya kiufundi katika mfumo wake wa uendeshaji.

Kusitishwa kwa huduma za kivuko hicho kunasababisha wenye magari wanaotaka kuingia au kutoka Kigamboni kulazimika kuzunguka njia ya Daraja la Mwalimu, kwa kuwa vivuko vilivyosalia vya MV Kazi na Sea Taxi vitatumika kuvusha abiria pekee.

Hili linakuja ikiwa imepita miezi mitano, zaidi ya muda ambao Temesa iliahidi kukamilika ukarabati wa MV Magogoni kilichopelekwa Mombasa kwa ajili ya matengenezo hayo yanayofanywa na mkandarasi wa Kampuni ya African Marine and General Engineering.

Februari 16, 2023 Serikali iliingia makubaliano na kampuni hiyo kukifanyia ukarabati kivuko hicho yaliyotarajiwa kukamilika Agosti, mwaka jana, lakini mpaka sasa kivuko hicho bado hakijarejea nchini.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Temesa, Lazaro Kilahala kuzungumzia suala hilo alijibu kuwa atakuwa na mkutano wa waandishi wa habari kesho Jumapili Januari 28, 2024.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 27, 2024 na Temesa imeeleza kusitishwa kwa huduma za kivuko cha MV Kigamboni ili kutoa fursa ya uchunguzi na matengenezo kufanyika katika mfumo wa uendeshaji, hivyo kuathiri huduma za usafiri hasa kwa wenye magari watakaolazimika kupita darajani..

Baadhi wa wakazi wa Kigamboni wameipokea taarifa hiyo kwa mitazamo tofauti wakitaka ipatikane suluhisho la kudumu kuwezesha watu kupata njia ya uhakika ya kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

 “Ni uamuzi wa busara kusitisha baada ya kuona kuwa kivuko kinahitaji matengenezo maana wangelazimisha huenda kingeleta maafa. Hata hivyo, ifike mahala lipatikane suluhisho la kudumu, hii adha tumekuwa tunakutana nayo mara kwa mara,” amesema Raphael Mtawa mkazi wa Kigamboni.

Shida Said amesema watumiaji wa magari wataingia kwenye changamoto ya kuzunguka umbali mrefu itakayowaongezea gharama.

“Mfano mimi naishi kanisani, mita chache baada ya kuvuka, natakiwa nizunguke darajani, hapa nitalazimika kuongeza mafuta maana mzunguko ni mrefu, ombi langu ikiwezekana hayo matengenezo yafanyike kwa haraka ili turudi kwenye maisha yetu ya kawaida,” amesema Shida.

Akizungumzia hilo, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amekiri kuwa hali ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni ni tete kwa kuwa utegemezi mkubwa ulikuwa kwenye kivuko cha MV Magogoni ambacho kina uwezo wa kubeba watu na magari kwa pamoja.

“Kigamboni kwa siku wanavuka watu 60,000 hadi 80,000 na magari 2,000, kwa taarifa hiyo ni kwamba, sasa kivuko kitabaki kimoja cha MV Kazi maana Seatax uwezo  wake ni kubea watu kati ya 100 hadi 150 hivyo hali ya usafiri kiukweli itakuwa changamoto.

“Wananchi wa Kigamboni tunachoona ipo haja ya sekta binafsi kuendesha huduma hizi za vivuko, Serikali ibaki kuwa msimamizi kuangalia ubora, usalama na ikusanye kodi lakini kazi ya uendeshaji iachwe kwa watu binafsi ili kupata ufanisi kwenye huduma,”amesema Dk Ndugulile.

Mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kwenye baraza la mawaziri, amesema kwa siku za usoni ni muhimu Serikali ikaona haja ya kujenga daraja ili kusiwe na utegemezi kwenye vivuko hasa katika kipindi ambacho uwekezaji mkubwa unaenda kufanyika bandari ya Dar es Salaam utakaotoa fursa kwa meli nyingi kuingia nchini.